Brenda Khasandi ,24, kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Allan Ongada ,26, ambaye alikosana naye Desemba mwaka jana.
Brenda alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika baada ya mumewe kumfukuza kwa kupokea simu yake alipopigiwa na mwanadada mwingine.
"Ilikuwa Desemba mwaka jana. Tulikuwa vizuri akaenda kazi kurudi jioni akaweka simu chini. Nikamuomba nikamwambia nataka kuingia online. Msichana akapiga simu mwendo wa saa tatu nikachukua, msichana kuskia sauti ya mwanamke akakataa," Brenda alisimulia.
Aliendelea, "Asubuhi msichana huyo akapiga simu akamwambia anadanganya hana bibi na ako naye. Hakuniuliza, alinyamazia tu na akafura. Nikaenda nikaambia mama yake. Alipoulizwa na mama yake hakueleza shida ni nini. Baadaye akaniambia niende nyumbani baada ya siku tatu atanifuata. Nilienda nikaambia cucu yake. Cucu yake alipomuuliza alisema ni mambo na simu, kwamba nashika simu yake. Nilisema tangu siku hiyo nimeacha kushika simu yake, bado hakunisamehe. Ilibidi niende nyumbani. Tangu niende nyumbani tunaongea kwa simu tu na mtoto anamlipia karo."
Brenda alisema licha ya kuahidi, mumewe hata hivyo hajawahi kumtumia nauli ama kumuendea takriban miezi saba baadaye.
"Siku tatu hazijawahi fika.Tunaongea anasema atatuma nauli akipata pesa. Tunaongea kama hana pesa, akipata pesa hatuongei... Najua hajaleta msichana mwingine, nilipigia ndugu yake akapatia watoto wakaniambia hajaleta mtu. Nilitoka tu na nguo tatu ambazo nilikuwa nimebeba. Aliniambia mbele ya cucu yake anataka niende siku tatu atulize roho. Baada ya siku tatu atanitumia nauli ama anikujie mwenyewe," Brenda aliongeza.
Allan alipopigiwa simu alithibitisha kwamba ni kweli aliahidi kumwendea mke wake baada ya siku tatu.
Hata hivyo, alidokeza kwamba kulitokea vikwazo vilivyofanya asitishe mpango wa kumrejesha mkewe.
"Sikumaanisha miaka tatu, nilimaanisha siku tatu. Zimepita lakini inategemea. Tulikosana kiasi na Brenda, nilimwamwambia aende nyumbani akaongee na watu wa nyumbani. Baadaye nikaanza kuskia maneno kidogo kidogo nikasema hayuko tayari ndio maana sikumfuata kwa haraka," Allan alisema.
Allan aliendelea kudai kuwa alifahamishwa mkewe alikuwa ameenda kujivinjari na mwanaume mwingine katika kilabu.
"Mimi sijakataa urudi na nyumba ni yako. Maneno naskia kwako zinaniudhi na zinanikera sana. Kuna ngoma ilikuwa Holo na ulienda. Najua ulikuwa na kijana ako na rasta. Niko na marafiki kila mahali, wakikuona wakaniambia nimeona bibi yako mahali. Niliona huko tayari, Ukikaa chini useme unataka kukaa utarudi," Allan alisema.
Brenda hata hivyo alipuuzilia mbali madai ya kujivinjari na mwanaume mwingine na kumshtumu mumewe kwa kusikiliza maneno ya watu.
"Niko na ushahidi wote kwamba alikuwa Holo. Ilikuwa ngoma na alienda na jamaa rasta. Rafiki yangu Geoffrey alinipigia simu akaniambia ameona Sharon," Allan alisema.
Brenda alimhakikishia mumewe kwamba yuko tayari kutulia kwa ndoa naye.
"Mimi ingekuwa singekuwa kurudi kwa nyumba yangu singekuwa namfuatilia kwa simu. Mimi nilimwambia kitambo niko tayari kubadilika lakini tubadilike pande zote ," Brenda alisema.
Allan alisema, "Mimi niko tayari arudi mradi tu abadilike. Atarudi end month nikilipwa mshahara."
Alimwambia mkewe, "Bado nakupenda na wewe ni mama ya mtoto wangu. Nakupenda na siwezi kuoa mwanamke mwingine. Kwa sasa niko mchafu vile uliniacha, nguo zangu ni chafu. Rudi utengeneze kwako."
Kwa upande wake Brenda alimwambia mumewe, "Bado nakupenda sana na wewe ndio baba ya mtoto wangu. Ndio maana nimeshinda kukufuatilia."