Jamaa ambaye alijitambulisha kama Kevin Otieno ,32, kutoka kaunti ya Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mchumba wake Emily Atieno ,24, ambaye alikosana naye siku chache zilizopita kufuatia mzozo wa mahusiano ya kando.
Otieno alisema uhusiano wake wa chini ya mwaka mmoja uliharibika mapema wiki hii baada ya mpenziwe kumpata akiongea na wapenzi wa zamani.
"Tumekuwa na mpenzi wangu kwa muda. Tumekuwa tukipanga mambo ya ndoa naye. Kuna siku nilimuita akakuja. Akakaa kaa kwa nyumba. Baadaye usiku niliacha simu, akapata meseji kwa simu. Nikamwambia hao ni watu wa kitambo wametuma meseji. Nilichukua simu, nikatoka nje akanifuata. Alitoroka saa saba ya usiku. Vile alitoroka nilijaribu kumfuatilia sikumpata. Naskia alienda kazi Nairobi," Otieno alisimulia.
Aliongeza, "Mmoja alikuwa ametuma meseji ya 'Hey' mwingine akasema 'Hey baby goodmorning'. Hao niliachana nao. Ni shetani tu alikuwa ananisukuma. Niliachana nao vile nilikuja nikaona naharibu. Hatuelewani naye."
Emily alipopigiwa simu, alithibitisha kwamba mpenzi wake alikuwa akizungumza na wapenzi wa zamani, jambo lililomfanya atoroke.
"Nilijaribu kukuongelesha, unakataa. Mimi niliamua tu hivyo," Emily alimwambia mpenziwe.
Otieno aliomba radhi huku akiapa kuwa tayari amebadilika.
"Ata niliacha kununua hizo sms. Nikinunua hizo sms ndo shetani huwa ananiingia. Nilibadilika sasa nataka tuishi pamoja. Niliacha hiyo maneno. Nimerudi kama mimi," Otieno alisema.
Emily alisema, "Ni sawa. Kama ulibadilika ni sawa.. Nampatia muda kwanza. Naweza kurudi saa hii na bado nipate hizo meseji. Ata kama niko mbali nitakuwa nakuja kama hujui. Pia anapenda kusikiliza maneno ya watu. Pia hiyo awache."
Baada ya Emily kukubali kumsamehe mpenziwe, Gidi alimfanya Otieno kuapa kwamba ameacha mambo ya mipango ya kando.
Wawili hao walikubaliana kuendeleza mahusiano yao ila Emily akamtahadharisha mpenziwe dhidi ya kurudia makosa yake.
Je, ushauri ama maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?