Mwimbaji na mtumbuizaji mashuhuri wa Kenya Ian Oure almaarufu Iyanii alikuwa mgeni wetu siku ya Jumanne katika kipindi cha Bustani la Massawe, kitengo cha Ilikuaje.
Akizungumza kwenye mahojiano, mwimbaji huyo wa kibao ‘Kifo cha Mende’ alifunguka kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo muziki, maisha, familia, mahusiano pamoja na mambo mengine.
Huku akizungumzia familia yake, mwimbaji huyo mwenye kipaji kikubwa alifichua kuwa yeye ndiye mzaliwa wa mwisho katika familia ya ndugu wanne.
“Dada
yangu anafanya kazi kwenye uwanja wa ndege, kaka yangu ni meneja wangu (ndiye
huyu hapa),” Iyanii alisema.
Aliendelea kufichua kuwa anatoka katika familia yenye mchanganyiko wa dini, ambapo baba yake ni Muislamu na mama yake ni Mkristo.
"Familia yetu ni nusu ya Waislamu, nusu ya Wakristo. Baba yangu amekuwa Mwislamu tangu alipokuwa mtoto. Familia yetu imekuwa nusu Waislamu na nusu Wakristo,” alisema.
Msanii huyo alifichua kwamba yeye binafsi alifuata kuwa Mkristo ilhali kaka yake na ambaye ni meneja Rashid ni Muislamu.
"Mimi huenda kanisa," alisema.
Mwimbaji huyo mahiri alibainisha kuwa babake amekuwa akiunga mkono sana muziki wake, lakini amekuwa akimshauri kuimba nyimbo za injili.
Pia alifichua kuwa ana uhusiano mzuri wa kikazi na kaka yake ambaye pia ni meneja wake kwani huwa wanazungumza sana na kujadiliana mambo.