logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Harusi ya kufana mwanawe Ghost Mulee: Undani wa Mambo yalivyokuwa

Mtangazaji Jacob Ghost Mulee, kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu harusi ya hivi majuzi ya mwanawe.

image
na Samuel Mainajournalist

Mahojiano28 February 2025 - 14:43

Muhtasari


  • Ghost alieleza kuwa ilikuwa fahari kubwa kwake kushuhudia mwanawe Jesse akifunga ndoa, kwani alimtazama akikua tangu akiwa mtoto mdogo.
  • Ghost alifichua kuwa mke wake, Carol Mulee, alihusika pakubwa katika mipango ya harusi hiyo maridadi ambayo ilifanyika kwa mpangilio mzuri.

Mwanawe Ghost Mulee alifanya harusi wikendi iliyopita

Kocha wa zamani wa Harambee Stars na mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob Ghost Mulee, kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu harusi ya hivi majuzi ya mwanawe.

Jesse Mutua ni mtoto wa kwanza wa Ghost, na ndiye wa kwanza kati ya ndugu zake kuchukua hatua kubwa ya kufunga ndoa. Alifunga pingu za maisha na mpenzi wake wa muda mrefu katika hafla ya kupendeza iliyofanyika jijini Nairobi wikendi iliyopita.

Akizungumza na mwanahabari Samuel Maina kuhusu hafla hiyo, Ghost alifichua kuwa harusi ilikuwa ya kufana na kila kitu kilienda kulingana na mpango.

“Harusi ilikuwa ya kufana. Kwanza nashukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu mpango ambao tulikuwa tumeweka, mikakati ilienda vizuri. Na nashukuru pia kamati ambayo ilikuwa husika kwa sababu kamati yenyewe iliongozwa na mwanadada. Ni msimamizi wetu wa kanisa, ndiye alifanya mambo mengi sana,” Ghost alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alieleza kuwa maandalizi yalichukua takriban miaka miwili, ikiwa ni pamoja na ziara kwa wakwe nchini Uganda.

Pia alifichua kuwa mke wake, Carol Mulee, alihusika pakubwa katika mipango ya harusi hiyo maridadi ambayo ilifanyika kwa mpangilio mzuri.

”Hii harusi ya kijana, mamake alihakikisha amefanya kila kitu vizuri. Ilikuwa harusi ambayo ilienda kulingana na ratiba, ilikuwa na desturi nzuri. MC alifanya kazi nzuri sana. Kila mtu alijihisi kama yuko nyumbani na chakula kilikuwa kingi, ungerudia mara kadhaa. Harusi ni chakula. Tulihakikisha kila mtu amepata chakula cha kutosha,” alisema.

Kuhusu nafasi yake katika maandalizi, Ghost alieleza kuwa alihusika zaidi kwa kutoa ushauri kwa mwanawe na kamati ya maandalizi.

”Kwenye harusi, kazi yetu ilikuwa ndogo tu. Ilikuwa ni kumpokea bi harusi kutoka kwa babake, kisha kijana akafunga ndoa. Nikasema ni sawa. Fursa yangu katika kamati haikuwa kubwa sana, lakini nashukuru kwa mchango wangu katika kuhakikisha mambo yamefanikiwa,” alisema.

Ghost pia alieleza kuwa ilikuwa fahari kubwa kwake kushuhudia mwanawe Jesse akifunga ndoa, kwani alimtazama akikua tangu akiwa mtoto mdogo.

“Nilipokuwa kanisani, walipofunganishwa pale, nilijihisi kama kutoa machozi. Si kawaida yangu kulia lakini nilikuwa natoa machozi ya furaha nikikumbuka safari ya maisha ya kijana wangu tangu azaliwe hadi sasa anafunga ndoa,” alisema.

Mtangazaji huyo wa redio alifichua kuwa wakati yeye na mkewe walifunga ndoa, mtoto wao Jesse alikuwa na umri wa miaka miwili pekee.

“Kumuona kijana mdogo amekua na sasa amefikia hatua ya kusema pia yeye anafunga ndoa, ilikuwa ni furaha kubwa sana kwangu,” alisema.

Ghost alimalizia kwa kumpa Jesse na mkewe heri njema katika ndoa yao, akiwataka waishi kwa amani.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved