
Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee amejawa na fahari baada ya mwanawe mmoja kupiga hatua kubwa maishani hivi majuzi.
Jesse Mutua Mulee alifunga pingu za maisha na mpenzi wake wa muda mrefu wikendi, na mtangazaji huyo mcheshi hakuweza kuficha furaha yake.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Ghost alimpongeza mwanawe na bintiye na kuwatambua kwa mafanikio hayo makubwa.
“Hongera Mr & Mrs Mutua Mulee kwa Siku yenu Kubwa,” Ghost aliandika kwenye Instagram.
Aliambatanisha ujumbe wake na video nzuri iliwaonyeshaa Jesse, mke wake, na wageni wengine kwenye harusi hiyo wakicheza densi kwa furaha.
Sote katika Radio Jambo tunawatakia Jesse na mkewe ndoa njema na yenye amani mbeleni.
Hatua hii inajiri wiki chache tu baada ya Ghost kusimulia hadithi ya kufurahisha sana kuhusu tukio la aibu lililotokea katika siku ya wapendanao iliyopita ambalo liliwahusisha wanawe.
Akizungumza wakati wa kipindi cha Januari, kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alifichua kuwa kisa hicho kilitokea katika msimu wa Valentines uliopita.
Ghost alisimulia jinsi alivyoitisha mkutano wa familia mnamo siku ya wapendanao, bila kujua kwamba wanawe wenye umri wa zaidi ya miaka 18 walikuwa na mipango yao wenyewe pamoja na mpenzi wao.
“Kuna siku nimewaambia vijana wangu kitu, na pia mimi nikajiona nilikuwa labda tu fala. Kuna siku ya Valentine fulani niliwapigia simu nikawaambia ‘Kesho tunaenda Valentine kama familia’. Wakanyamaza, kesho yake wakaniandikia barua wakaniambia, ‘Baba, si uko na mpenzi wako, mama yetu, mpeleke yeye, pia sisi tuna wapenzi. Wewe tupatie tu pesa pia sisi tukajishughulikie, uliona wapi Valentine ya familia kama mtu amefikisha miaka 18?” Ghost alisimulia.
Mtangazaji huyo mahiri wa redio alikiri kwamba tukio hilo lilimwacha akiwa na aibu lakini hakuwa na budi ila kuheshimu maamuzi ya wanawe.
Ghost alitumia fursa hiyo kuwasihi wazazi wengine kuwa wanawaelewa watoto wao na daima kuheshimu maamuzi yao binafsi.
“Nilijiona fala sana, sasa kutoka hiyo siku huwa nawauliza wako na mpango gani. Huwa nawauliza kama wanapatikana,” alisema.
“Kama mzazi, lazima uelewe kwamba kila mtoto wako na utu wake. Lazima ujue kwamba huwezi kuwasimamia watoto wako tena wakishafikisha miaka 18. Mimi niliwaambia baada ya kufikisha miaka 18, wajue kwamba wao ni watoto wa serikali.
Wazazi wanafaa kuwa wanafahamu watoto wao, na watoto pia wafahamu wazazi wao. Hata kwa Bibilia, wazazi walikuwa wananakosana na watoto wao na pia watoto wanakosana na wazazi. Cha muhimu ni kuwe na heshima,” aliongeza.
Akizungumzia yaliyompata mtangazaji mwenzake, Gidi alimweleza kuwa alichokifanya ni cha aibu kwa kweli.
“Wewe Mulee pia wewe ulichoma bana, unachunga vijana wa miaka 18 unataka kuwapeleka Valentine na wako na wapenzi?,” Gidi alimwambia mwenzake.
Ghost aliweka wazi kuwa sasa anaelewa haiba ya watoto wake kutokana na kutokana na kutembea sana.
"Kwa sababu ya exposure, vijana wangu, kila mtu namelewa, najua personality yake," alisema.