Jamaa ambaye alijitambulisha kama Kevin Ochieng Omondi ,30, kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Beatrice Akoth ,25 ambaye alikosana naye mwishoni mwa mwaka jana.
Kelvin alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwezi Desemba baada ya kuzozana naye kuhusu ulevi.
"Nilienda kutafuta kazi, nikakosa. Nikaingia kwa marafiki nikapiga karobo, nikarudi kama nimelewa kabisa. Nikaingia nikalala. Kutoka nikapata mke wangu amechukua kila kitu ameenda," Kelvin alisimulia.
Aliongeza, "Nilimuoa akiwa na watoto wawili. Nilikuwa ninawashughulikia. Akitoka alienda na watoto. Tulikuwa tunazungumza ila sasa ameniweka blacklist. Tuliongea siku ya Jumanne lakini sioni kama ako na roho ya kurudi. Alisema atarudi akipenda. Nilikuwa nataka ashawishiwe arudi kwa sababu nampenda. Tayari nimebadilika, nishaanza kanisa."
Beatrice alipopigiwa simu mwanzoni alikana kumfahamu jamaa huyo kabla ya kuweka wazi kuwa hataki mambo yake.
"Huyo jamaa mimi simjui!" Beatrice alisema.
Kelvin alijitambulisha na kumwambia, "Hayo yote nilikukosea naomba unisamehe urudi."
Beatrice naye alijibu, "Nilikwambia vizuri mambo yako sitaki kuskia," kabla ya kukata simu.
Alipopigiwa simu mara ya pili, Beatrice alisema, "Aniache kabisa na ajipe shughuli."
Kelvin alilialamikia hatua ya mwanadada huyo kumdanganya angerudi na kumtaka asiwe anampigia simu.
"Nilikuwa nadhani kuna ukweli. Endlea na maisha yako na numba yangu usinipigie. Ulikuwa unataka kunikula kula pesa yangu.Juzi nilimtumia 200 akasema kichwa inauma anataka kununua dawa," alisema.
Beatrice alijibu, "Hiyo ni kawaida ya msichana lazima nikule fare yako. Msichana akikula 200, hiyo ni pesa? 200 inakuwanga pesa? 200 hata haiwezi nunua mafuta yangu ya kupaka!"
Kelvin alishangaa na kumuuliza, "Kwani ni matawi? Kwani unapaka mafuta ya pesa yangu. Si ungenitumia thao? naweza kurudishia saa hii. Wewe endelea kunywa pombe yako na bangi, achana na mimi."
Aliongeza, "Juzi nilimkuta na mwanaume mwingine akanidanganya ni kakake. Alikuwa anataka kuniharibia wakati. Heri nitafute mwingine wa kuishi."
Je, ushauri wako kwa wawili hao ni upi?