Patanisho: 'Nilinyoa dreadi nikifikiri ndoa itaimarika ila ikaharibika' Jamaa asimulia masaibu ya ndoa yake

Jamaa huyo alidai kuwa walitengana na mkewe wa miaka tatu mwezi wa Aprili mwaka huu baada yake kuambiwa maneno ya fitina na wanawake wengine.

Muhtasari

•Boniface Baraza, 31, kutoka Malava alidai kuwa walitengana na mkewe wa miaka tatu mwezi wa Aprili mwaka huu baada yake kuambiwa maneno ya fitina na wanawake wengine.

•Alisema kuwa alikuwa na rasta hapo awali ila akaamua kuzinyoa akitumai kuwa ndoa yake itaimarika ila akasema iliendelea kuharibika zaidi.

ghost
ghost
Image: RADIO JAMBO

Kwenye kitengo cha patanisho siku ya leo, Jumatano Julai 28, jamaa mmoja alitaka kupatanishwa na bibi yake aliyedai kamuacha kwa sababu ya fitina.

Boniface Baraza, 31, kutoka Malava alidai kuwa walitengana na mkewe wa miaka tatu mwezi wa Aprili mwaka huu baada yake kuambiwa maneno ya fitina na wanawake wengine.

"Tulikuwa hatuelewani vizuri pale kwa nyumba, nikatoka nikaenda matanga peke yangu. Ikawa majirani wakamwambia kuwa nilioa mwanamke mwingine nikaenda naye nyumbani nikamuacha kwa nyumba" Baraza alisema. 

Jamaa huyo pia alikiri kuwa kulikuwa na tatizo la pesa kwenye boma lake na hiyo ilikuwa sababu moja ya ugomvi uliokuwepo kati yake na bibiye.

"Kurudi nilipata amechukua  nyumba ingine amehama... huwa tunaongea juu mtoto ananihitaji huwa napeleka mahitaji huko... nimemuulizia anasema tu kesho kesho. Kuna wakati aliniambia kuwa pia alikuwa analipiza kitu nilikuwa namfanyia, sijui saa hii imefikia wapi." Aliendelea kusema.

Baraza alidai kuwa anampenda mke wake sana ila alikuwa amekataa kabisa kumuelewa.

Alisema kuwa alikuwa na rasta hapo awali ila akaamua kuzinyoa akitumai kuwa ndoa yake itaimarika ila akasema iliendelea kuharibika zaidi.

"Nilibaki kipara  mpaka kichwa siku hizi inauma tu kila siku. Mazungumzo ilikosekana kila siku" Jamaa huyo alisema.

Kwa upande wake mkewe alidai kuwa alimtaka mumewe aende ajitambulishe kwa wazazi wake kwanza.

"Nilimwambia tu aende aone wazazi  nyumbani kwetu. Hiyo tu ndio suluhisho alafu tutarudiana.. Hajajitambulisha hata kwetu na tuna kijana wa miaka tatu" Mkewe alidai.

Mwanaume huyo alidai kuwa alikuwa na nia ya kuenda kwa kina bibi ila akampa vitisho kuwa akienda huko angepokea kichapo.

"Mimi nilikuwa naenda kwao lakini kitu ilisababisha nikakosa kuenda ni kwa sababu aliniambia tu nikikanyanga kwao viboko tu na mafimbo ndizo zitakuwepo" alisema jamaa huyo.

Hata hivyo bibi yake alikanusha madai kuwa kulikuwa na njama ya kumpiga mumewe pindi atakapofika kwao.

Wawili hao waliagana kuwa wangezungumza na kupanga mipango ya kurudiana.