Patanisho: "Bwanangu hataki nimtembelee, nilimpata na Ann, Phylis, Petra, Flo" Mwanadada asimulia masaibu ya ndoa yake

Muhtasari

•Bi Adhiambo alifichua kuwa Oduor alimuoa akiwa na umri mdogo wa miaka 14 na kwa kipindi cha miaka sita ambacho wamekuwa kwa  ndoa  mumewe hajawahi kuwa wazi kwake.

•Mwanadada huyo pia alifichua kwamba amewahi kumnasa mumewe akiwa na mipango wa kando wanne tofauti ila bado hataki kutupilia ndoa yake mbali kwani anampenda sana Oduor

•Adhiambo pia alitaka mumewe awe akimtimizia mahitaji yake ya kitandani akidai kwamba alikuwa amemtelekeza sana.

Ghost na Gidi
Image: Studio

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi ya Jumatano Bi Skovia Adhiambo 21, kutoka Homabay alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Albert Oduor 30, ambaye wamekuwa kwa ndo naye kwa miaka sita na kubarikiwa na watoto wawili.

Bi Adhiambo alimshutumu mumewe kutokuwa mwaminifu , kutoa siri zao za ndoa nje, kufunga simu yake kwa nambari za simu na kumlazimisha kujiunga na kanisa la Katoliki licha ya yeye kutokuwa wa dhehebu hiyo.

"Bwanangu hataki hata nimtembelee mjini. Kuna siku nilipanga kwenda huko kama hajui nikapata amehama. Pili wazazi wake wanaingilia ndoa yetu kabisa. Juzi nilienda kuomba kwa kanisa ingine kwa kuwa mimi si wa Katoliki na babake akanigombanisha. Nilipopigia bwanangu simu azungumze na babake pia yeye akanigombanisaha akasema eti hataki mambo ya kanisa lingine isipokuwa la Katoliki.. Tatu ameweka 'pattern' kwa simu na wakati tunapokuwa naye kwa nyumba nikimuuliza anakataa kuniambia. Hiyo ndiyo inaleta shida kati yetu" Alisema Adhiambo.

Bi Adhiambo alifichua kuwa Oduor alimuoa akiwa na umri mdogo wa miaka 14 na kwa kipindi cha miaka sita ambacho wamekuwa kwa  ndoa  mumewe hajawahi kuwa wazi kwake.

Mwanadada huyo pia alifichua kwamba amewahi kumnasa mumewe akiwa na mipango wa kando wanne tofauti ila bado hataki kutupilia ndoa yake mbali kwani anampenda sana Oduor.

"Aliweka pattern kwa simu baada yangu kugundua kwamba ako na mipango ya kando. Wa kwanza alikuwa anaitwa Ann, wa pili alikuwa anaitwa Phylis, wa tatu alikuwa anaitwa Petra na wa nne alikuwa anaitwa Flo. Mpaka anawatumia picha zake akiwa hana shati. Hata nikiongea na yeye ama aongeleshwe na wazazi hataki kubadilika. Nampenda sana yeye ni baba wa watoto wangu" Alisimulia Adhiambo.

Adhiambo alisema kwamba alipatana na mumewe akiwa katika kidato cha pili baada ya wazazi wake kuaga na kuachwa akisekea mikononi mwa mama wake wa kambo.

Mwanadada huyo alitaka mumewe aache kufunga simu yake, aachane na mambo ya mipango ya kando, aache kutoa siri zao za ndoa nje na asimlazimishe kuenda kanisa ya Katoliki.

Adhiambo pia alitaka mumewe awe akimtimizia mahitaji yake ya kitandani akidai kwamba alikuwa amemtelekeza sana.

Bwana Oduor alipopigiwa simu alikiri kwamba aliwahi kunaswa na mipango ya kando ila akadai kuwa alikuwa ameacha tabia zile. Alisema kwamba ako na shida nyingi na mkewe ila  hangependa kuzifichua  hewani.

Oduor  alipoulizwa kuhusu suala la kufunga simu ili mkewe asiweze kumchunguza alidai kwamba Bi Adiambo pia amefunga simu yake na takriban 'pattern' 20.

Oduor hakutaka kuzungumzia masaibu ya ndoa yake  zaidi na alikata simu wakati kipindi kilikuwa kinaendelea.

Gidi alimshauri mwanadada huyo aondoke pale arejee nyumbani kwao na apatie mumewe masharti kabla yake kurudi.

Je una ushauri upi kwa Adhiambo?