Patanisho: "Bwanangu alitaka nimlipie rent, karo, chakula" Mwanamke azungumzia tabia za mumewe zilizomsukuma atoke kwa ndoa

Muhtasari

•Jack 31, alisema kwamba walikosana na mkewe baada yake kukosa kazi na tangu wakati ule amekuwa akisononeka sana.

•Bi Mary alidai kwamba Jack alikuwa amegeuka kuwa kupe kwake kwani alimtaka yeye awajibikie mahitaji yote ya nyumbani na ndio maana akachoka na kuamua kuondoka.

•Mary alidai kwamba kando suala la pesa mumewe alikuwa mraibu wa pombe na bangi, madai ambayo Jack alikanusha.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost asubuhi' siku ya Alhamisi kitengo cha Patanisho, Bwana Jack kutoka Kayole alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mary 28, ambaye walitengana mwezi Juni mwakani.

Jack 31, alisema kwamba walikosana na mkewe baada yake kukosa kazi na tangu wakati ule amekuwa akisononeka sana.

Wawili hao wamekuwa kwa ndoa kwa kipindi cha miaka sita na wamebarikiwa na watoto wawili pamoja.

"Ningependa kuomba bibi yangu msamaha.. tulikosana naye mwezi Juni 2021 baada yangu kukosa kazi kisha akaniambia nishughulikie familia. Saa hii nasononeka moyoni" Jack alisema.

Jamaa huyo alisema kwamba  kwa sasa mkewe amekatiza mawasiliano kati yao licha ya kuwa aliweza kupata kazi.

"Saa hii nilishapata kazi ingine na nikamwambia ila alisema nikae na kazi zangu hataki mambo yangu" Alieleza Jack.

Jack pia alifichua kwamba alimpiga mkewe 'kidogo' wakati walikuwa wanazozana kuhusiana na hali yake ya kukosa ajira.

Bi Mary alipopigiwa simu alidai kwamba Jack alikuwa amegeuka kuwa kupe kwake kwani alimtaka yeye awajibikie mahitaji yote ya nyumbani na ndio maana akachoka na kuamua kuondoka. Mary pia alifichua kwamba mumewe alikuwa mkatili mara kwa mara.

"Anataka kila kitu nimfanyie, nimlipie kodi ya nyumba, nimnunulie chakula mpaka nalipa karo ya shule. Ilifika mahali akasema kwamba atanidunga na kisu, ikafika mahali nikasema mimi sitaweza. 

Hata wakati alipoteza kazi nilikuwa naenda kwa dadangu nanunua chakula tunakula na yeye. Hata alipopata kazi si eti ananisaidia, mimi mwenyewe nashughulikia kila kitu" Mary alisema.

Jack alijitetea kwa kusema kwamba alipopata kazi alikuwa anamrejeshea mkewe pesa ambazo alikuwa ametumia baada yake kupokea mshahara.

Mary kwa upande wake alidai kwamba pesa ambazo mumewe alikuwa akimrejeshea zilikuwa za kodi ya nyumba tu na hakuwa anagharamia mahitaji mengine.

"Alikuwa anarejesha za kodi ya nyumba tu baada ya kupokea mshahara. Akishanipatia ya nyumba hakuwa ananipatia ya mahitaji mengine kama chakula. Mimi mwenyewe nilikuwa nashughulikia kila kitu. Nikamwambia hayo maisha sitaweza. Mimi nlimwambia asonge mbele na maisha yake" Mary alisema.

Mary alidai kwamba kando suala la pesa mumewe alikuwa mraibu wa pombe na bangi, madai ambayo Jack alikanusha.

"Mimi ata sijawahi vuta bangi. Pombe nilikunywa wakati alianza kuleta vurugu. Akiona nimelewa ama nikitembea na vijana anasema eti huwa navuta bangi. Mimi sijawahi vuta" Jack alijitetea.

Licha ya juhudi kubwa za kushawishi Mary kumrudia mumewe, mwanadada huyo alisisitiza kwamba alikuwa amechoshwa na ndoa hiyo na hangeweza kumpatia nafasi ingine.