Patanisho: "Nilijaribu kuoa mwingine nikaona heri shetani niliyemzoea" Jamaa ajuta kufukuza mke wa kwanza

Muhtasari

•Cliff alidai kwamba walikosana na mkewe alipomdanganya kwamba ameenda kutembelea mjomba wake ila baadae akagundua kwamba alikuwa ameenda kupeleka dadake kuona mpenzi wake kwa kipindi cha siku mbili.

•Baada ya ndoa yao kuvunjika, hali ya upweke ilimfanya Cliff atafute mwanamke mwingine na akajaribu ndoa naye ila haikudumu. Alisema kuwa alikuwa anampeza sana mkewe wa kwanza

Cliff alikiri kuwa alikuwa amepata funzo kubwa kufuatia utengano wao na kudai kwamba alikuwa akijuta sana.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost asubuhi' kitengo cha Patanisho, Bwana Cliff Omondi (30) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Cindy Awour (25)  ambaye walitengana mwezi Desemba 2019.

Kwenye ujumbe wake Cliff alieleza kwamba walikuwa kwa ndoa na Cindy kwa kipindi cha miaka mitatu na walikuwa na mtoto mmoja.

Cliff alidai kwamba walikosana na mkewe alipomdanganya kwamba ameenda kutembelea mjomba wake ila baadae akagundua kwamba alikuwa ameenda kupeleka dadake kuona mpenzi wake kwa kipindi cha siku mbili.

"Dadake mkubwa alikuja nyumbani alafu wakanidanganya kwamba wanaenda kutembelea mjomba wao. Wakati nilipigia mjomba wake aliniambia kwamba hawakuwa wameonekana huko ndio nilikasirika. Wakati alirudi ndio aliniambia kwamba alikuwa amepeleka dadake kutembelea mpenzoi wake kwa siku mbili. Nikaona kama kulikuwa na mchezo mwingine hapo ndani" Cliff alisimulia.

Baada ya kugundua kuwa mkewe alikuwa amemdanganya kuhusiana na safari yake Cliff alijawa na ghadhabu na akaambia mkewe arudi amahali alikuwa ametoka.

Mkewe hakusita kuondoka pale nyumbani kwake na akaondoka kuelekea jijini Nairobi.

Baada ya ndoa yao kuvunjika, hali ya upweke ilimfanya Cliff atafute mwanamke mwingine na akajaribu ndoa naye ila haikudumu. Alisema kuwa alikuwa anampeza sana mkewe wa kwanza.

"Hapo mbeleni nilijaribu kuoa ila nikapima hewa nikaona afadhali ata huyo bibi yangu arudi badala ya kuanza maisha na bibi mwingine.  Niliona afadhali shetani ambaye nimemzoea" Cliff alisema

Cindy alipopigiwa simu alisema kuwa alikuwa tayari kushiriki mazungumzo na mumewe ili wapange mikakati ya kurudiana.

"Nataka tukae chini na yeye tuongee.. kuna dalili tunaweza kurudiana" Cindy alisema.

Cliff alikiri kuwa alikuwa amepata funzo kubwa kufuatia utengano wao na kudai kwamba alikuwa akijuta sana.

"Ni funzo kubwa. Nimetafakari nikaona heri kurudia mke wa kwanza. Kabla ya kujaribu huwezi jua lakini baada ya kujaribu uone mbele kuna giza baaass. Niliona heri mke wangu wa kwanza" Cliff alisema.

Gidi alishauri wawili hao waketi chini na kujadiliana kuhusu mikakati ya kurudiana.