'Nilipata bwanangu na mwanamke, nikakasirika nikamuachia mtoto wa miezi 6', Wanandoa wasimulia masaibu yaliyokumba ndoa yao ya miaka 5

Muhtasari

•Alice alisema kwamba alikuwa ameenda kufanya shughuli yake ya kawaida ya kuuza mboga ila siku hiyo akarudi mapema kuliko kawaida yake ndipo akapata mumewe akiwa na mwanadada mwingine kwa nyumba.

•David alisisitiza kwamba mwanamke ambaye mke wake alikuwa amempata naye kwa nyumba alikuwa mwanachama mwenzake ila hakuwa mpango wake wa kando.

•David alikataa abadan katan kurudiana na mkewe akidai kwamba hangeweza kuishi na mwanamke ambaye alikuwa amebadilisha mienendo.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost asubuhi' kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Alice Muhonja alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe aliyetambulisha kama David.

Alice alisema kwamba walitengana na mumewe mwezi Januari mwaka huu kufuatia mzozo wa mapenzi ambao ulikatiza ndoa yao ya miaka mitano.

Mwanadada huyo alidai kwamba alimfumania mumewe na mwanamke mwingine ndani ya nyumba yao, wakazozana kwa muda kisha akakasirika akaondoka na kumuachia mtoto wao wa miezi sita.

"Nilikuwa nimeenda kibarua nikampata na mwanamke kwa nyumba. Nilipomuuliza aliniambia eti alikuwa mama wa chama. Mimi nikamwambia sijaelewa hayo nikasema hayo si kweli. Nilipomuuliza nikaona kama kwamba anataka kubadilisha sura yake nikakasirika nikaingia kuchukua manguo zangu nikamuachia mtoto wake mi nikaenda" Alice alisimulia.

Alice alisema kwamba alikuwa ameenda kufanya shughuli yake ya kawaida ya kuuza mboga ila siku hiyo akarudi mapema kuliko kawaida yake ndipo akapata mumewe akiwa na mwanadada mwingine kwa nyumba.

Hata hivyo alisema kuwa alikuwa amejuta hatua aliyokuwa amechukua kutokana na hasira na kudai angependa kurudiana na David.

David alipopigiwa mara ya kwanza alisita kuzungumza punde baada ya kuelezwa kwamba ni Alice alikuwa anamtafuta.

David hata hivyo alikubali kuzungumza alipopigiwa mara ya pili ila aliskika kajawa na ghadhabu kweli.

Alisisitiza kwamba mwanamke ambaye mke wake alikuwa amempata naye kwa nyumba alikuwa mwanachama mwenzake ila hakuwa mpango wake wa kando.

David alidai kwamba baadae aligundua mienendo ya mama ya mtoto wake ilibadilika baada ya kuondoka kwake, jambo ambalo lilimsikitisha sana.

"Aliniachia mtoto kwa kiti akaenda. Alienda kwao akakaa wiki moja kisha akaondoka akaenda kazi Eldoret kwa hoteli moja. Mimi kumfuata nikapata amebadilika. Nilipata akiwa amejipaka rangi, ametengeneza nywele, amevaa long knee, amevaa leather jacket, amevaa viatu vya open, amepaka midomo rangi, amengara.. mimi nikaachana na yeye. Alikuwa anafanya kazi kwa baa" David alisimulia.

Kuona jinsi Alice alikuwa amebadilisha mienendo, David alibadilisha uamuzi wake wa kumrejeshea mkewe mtoto na akaamua kumpelekea mama yake.

Hata hivyo Alice alipuuzilia mbali madai kuwa alikuwa anafanya kazi kwa baa na kusisitiza kwamba alikuwa amepata kazi kwa boma ya mtu.

David alidai kwamba Alice alikuwa na uhusiano na bwenyenye mmoja mjini Eldoret na kusema kuwa alikuwa amewaona pamoja wakiwa ndani ya gari aina ya Prado.

"Wewe ishi na huyo mdosi wako. Kuleni raha yenu mimi usiniletee mchezo!" Kwa hasira David aliambia mkewe.

David alitilia shaka madai ya Alice kwamba bwenyenye ambaye Alice alikuwa anaishi naye alikuwa mdosi wake na kudai kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.

"Yeye saa hii ni mlevi anakunywa pombe, anafanya kazi kwa baa. Kila wakati anakunywa Tusker, Pilsner na zingine kali. Tajiri gani mtu mwenye hana bibi?? Tajiri yupi mnaishi naye kwa nyumba watu wawili??" David ambaye matamshi yake yalikuwa yamejawa na hasira alisema.

David alikataa abadan katan kurudiana na mkewe akidai kwamba hangeweza kuishi na mwanamke ambaye alikuwa amebadilisha mienendo.

'Yeye ashikane na mdosi wake , afanye mambo yake, afanye starehe zake, ajipondoe, ang'are, aende mbele barabara bado ni refu. Lakini stori zangu awache kuangalia nyuma aangalie mbele" Alisema David.

David pia alikataa ombi la mkewe la kurejeshewa watoto alee mwenyewe badala ya kuwaachia mama mkwe.