Patanisho: 'Mwanadada niliyepata mtoto naye alipigia mke wangu akamwambia aniarifu nitume karo', Jamaa asimulia alivyotemwa na mkewe

Muhtasari

•Benson Simiyu (30) alidai kwamba mkewe aliyetambulisha kama Rose aliondoka nyumbani baada ya kupokea simu kutoka kwa mwanadada ambaye alimuarifu aambie bwanake amtumie karo ya shule ya mtoto ambaye walipata pamoja.

•Rose alipogundua kwamba mumewe alikuwa amenyemelea nje alijawa na hasira na kizaazaa kikubwa kikaanza katika boma ile. 

•Rose alisema kwamba jambo hilo lilimsikitisha sana kuona kwamba bwanake alikuwa ameficha ukweli kwa muda mrefu.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost asubuhi' kitengo cha Patanisho, jamaa alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe ambaye alimuacha baada ya kugundua kwamba ako mtoto nje ya ndoa.

Benson Simiyu (30) alidai kwamba mkewe aliyetambulisha kama Rose aliondoka nyumbani baada ya kupokea simu kutoka kwa mwanadada ambaye alimuarifu aambie bwanake amtumie karo ya shule ya mtoto ambaye walipata pamoja. 

"Kuna mwanadada ambaye tulipata mtoto naye huko nje. Wakati alipiga simu mke wangu akapokea na akaambiwa kwamba mtoto alikuwa amefukuzwa shule eti nitume karo. Alipoambia hivo akakasirika na kuuliza mbona sijawahi kumwambia kwamba niko na mtoto nje" Bwana Simiyu alisema.

Simiyu alidai kwamba bado hakuwa amepata ujasiri wa kuarifu mkewe kuwa alikuwa amepata mtoto nje  licha ya kuwa kwa ndoa tayari.

Benson na Rose wamekuwa kwa ndoa kwa kipindi cha miaka saba na tayari wamebarikiwa na watoto wawili.

"Mtoto nilipata nje kama tayari nimeoa huyu mwenye tumekosana naye" Benson alikiri.

Rose alipogundua kwamba mumewe alikuwa amenyemelea nje alijawa na hasira na kizaazaa kikubwa kikaanza katika boma ile. 

Simiyu alikiri kuwa alimzaba mkewe kofi kutokana na hasira walipokuwa wanazozana kuhusu suala la mtoto huyo.

"Nilimchapa kofi moja tu alafu akakasirika huku akiuliza kwa nini nilikuwa nimemfanyia yale na sijawahi kumwambia. Jumapili ndio akatoka akaenda kwao" Alisema Simiyu.

Simiyu alidai kwamba baada ya hayo alitumia mpango wake wa kando karo ya shule ya mtoto wao ila bado hakuwa amewasiliana na mumewe.

Bi Rose alipopigiwa simu alithibitisha yote ambayo yalitukia ndipo akafanya maamuzi ya kumtema mumewe wiki moja iliyopita.

"Tumekaa na yeye miaka saba na hajawahi niambia eti ako na mtoto nje. Nilikuwa namuuliza hakuwa anakubali kuniambia. Huyo msichana ndiye alinipigia simu akaniambia eti 'ambia bwanako nataka karo ya shule'. Nikamuuliza karo ya nini.. akauliza kwani bwanangu hajawahi niambia eti wamepata mtoto pamoja. Sasa mimi nikamuuliza alafu hata kujibu ikawa shida" Rose alisema.

Rose alidai kwamba ilichukua muda kushawishi mumewe amwambie ukweli na hatimaye akafichua kwamba ako na mtoto wa miaka mitatu nje. Hata hivyo alitilia shaka jambo hilo shaka kwani alishindwa vile mtoto wa miaka tatu tayari  alikuwa ameanza masomo.

"Mimi nilikasirika nikaenda nyumbani. Kwanza alinipiga ndipo nikatoka nikaenda nyumbani" Rose alisema.

Simiyu alijitetea kwa mkewe na kumuomba msamaha akidai kwamba alikuwa anajaribu kutafuta nafasi mwafaka ya kumuarifu kuhusu mtoto huyo.

Rose alisema kwamba jambo hilo lilimsikitisha sana kuona kwamba bwanake alikuwa ameficha ukweli kwa muda mrefu.

Alifichua kwamba mumewe walipokuwa wanazozana mumewe alimwambia kwamba kunao wasichana wengi ambao wangefuata na kesi kama ile ile.

"Alisema nitegee wengi wanakuja eti hiyo ni kidogo" Rose alisema.

Kwa upande wake Simiyu alisema kwamba matamshi hayo yalikuwa yamesababishwa na hasira na kuhakikishia mkewe kuwa hana watoto wengine nje.

"Si eti kuna wengine. Nilikuwa naongea nikiwa na hasira wakati aliniuliza. Hasira aliponishika nikaamue wacha nimwambie eti kuna wengi wanakuja" Alisema Simiyu.

Hata hivyo Rose alikubali kumsamehe mumewe na kumsihi arekebishe tabia zake ili waweze kuishi kwa  amani.

"Mimi sina shida na yeye kwa sababu tumezaa na yeye watoto wawili lakini ajirekebishe. Hii dunia ni mbaya. Tumetoka mbali na yeye, nikikuja hakuwa na chochote. Siku hizi vile ameanza kupata ndio ikakua shida" Rose alisema.

Wawili hao walikubaliana kurudiana huku Simiyu akikubali kuenda kwa kina Rose ili amchukue warejee naye nyumbani.

Je, una ushauri upi kwa wawili hao?