Patanisho: "Bwanangu aliambia yeye ni jambazi, alisema atatuma vikosi kutupiga usiku" Mwanadada asimulia maovu ya mumewe

Muhtasari

•Kulingana na Dennis, kosa la pekee ambalo aliwahi tendea mkewe ni kujitosa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanadada mwingine mwaka uliopita na hata wakapata mtoto pamoja. 

•Kando na suala la mipango wa kando, Phylis alifichua kwamba mumewe alikuwa na mazoea ya kutumia shangazi yake jumbe chafu na kupatia familia yake vitisho.

•Phylis alisema kwamba aliporudi kwao Dennis alianza kumpigia simu huku akimpatia vitisho kuwa angetuma magenge kushambulia familia yake iwapo wangekataa kumpatia mtoto wake.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost asubuhi' kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Dennis (28) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Phylis Atieno (26).

Dennis alisema kwamba ndoa yake ya miaka mitatu ilifika kikomo wiki iliyopita kwa sababu asizozifahamu kwani mkewe aliondoka tu bila kumuarifu na kumuachia mtoto wao mdogo.

Alidai kuwa juhudi za kumfikia mkewe hazijaweza kufua dafu baada ya hayo kutokea kwani tayari amekatiza mawasiliano kati yao.

Kulingana na Dennis, kosa la pekee ambalo aliwahi tendea mkewe ni kujitosa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanadada mwingine mwaka uliopita na hata wakapata mtoto pamoja. 

Dennis hata hivyo alidai kwamba walisuluhisha mzozo huo kitambo na tayari mkewe alikuwa amemsamehea.

"Nilikuwa na msichana na nikapata naye mtoto. Nilimuomba msamaha ikaisha. Huyo msichana ata huwa hatuongei na sijui mahali alienda. Tuliongea kwa nyumba kama bibi na bwana" Dennis alisema.

Phylis alipopigiwa simu alikuwa na mengi ya kufichua kuhusu ndoa yake ambayo Dennis alikuwa ameficha.

Kando na suala la mipango wa kando, Phylis alifichua kwamba mumewe alikuwa na mazoea ya kutumia shangazi yake jumbe chafu na kupatia familia yake vitisho.

Phylis alisema kwamba aliporudi kwao Dennis alianza kumpigia simu huku akimpatia vitisho kuwa angetuma magenge kushambulia familia yake iwapo wangekataa kumpatia mtoto wake.

"Bwanangu ako na mambo machafu. Nilipoondoka alisema eti loan ilifanya nikaondoka pale. Nilipofika nyumbani alianza kutumia shangazi yangu jumbe chafu chafu. 

Jambo la pili alianza kututishia usiku. Aliniambia yeye ni jambazi kama shangazi na nyanya yangu wanaskia. Alisema tumrudishie mtoto na iwapo hatutarudisha ako na vikosi ambazo zitakuja kwetu usiku vituchape na tuwapatie mtoto kwa lazima. Nyanyangu na shangazi yangu wakaogopa wakaniambia nirudishe mtoto kwani walihofia kupigwa usiku" Phylis alisema.

Phylis alifichua kwamba mumewe alikuwa amemdhalilisha na kumkosea heshima kabisa hata kiwango hata aliwahi mwambia aolewe na babake.

Alisema kwamba wamekuwa wakizozana kwa muda ila amekuwa akivumilia tu lakini ilifikia wakati hata nyanyake akamuonya dhidi ya mumewe.

Phylis alieleza  kuwa alihofia jambo mbaya lingemtendekea akiwa pale kwa Dennis kwani aliwahi mwambia kuna silaha ambayo ameficha juu ya mlango.

"Mimi siwezi kaa na jambazi. Sijui kama utanidunga kisu. Uliniambia eti vvile tumekaa na wewe sijawahi angalia juu ya mlango, mimi sijui kama uliweka bunduki hapo na utaitumia kunia. Mimi sasa nilikataa tamaa nikaenda na nikapata kazi. Mimi sasa sitaki maneno mingi" Phylis aliambia Dennis.

Alisema kwamba kilichomkera zaidi na kumfanya afanye uamuzi wa kuondoka ni kitendo cha mumewe kupiga picha na mwanadada mwingine na kupakia kwenye mtandao wa Facebook.

Phylis alisema kuwa alimpenda sana mumewe ila Dennis mwenyewe hakuwa anamuonyesha mapenzi yoyote.

"Denno umeniharibu kwa kila kitu. Mpaka familia yangu wamebaki wakinidharau. Ni mambo mangapi umenifanyia.. Kilichopandisha hasira hata si yule msichana ulizaa naye mtoto. Kuna yule mwenye mlipiga naye picha ukaweka Facebook. Ni lini mimi nilipiga na mwanaume nikaweka Facebook. Mimi nakuvumilia tu! Ni kwa nini umenidharau hivo?

Mimi nilikuwa nakupenda sana. Nilikuwa nakupenda lakini mapenzi yako hukunionyesha. Hata nilikuzalia mtoto lakini unatoka nje  unaenda kuzaa mtoto. Ni nini ulikosa ukaenda kutafuta nje. Kwa nini unanifanya hivo Dennis?" Phylis alilia.

Dennis hata hivyo alipuuzilia madai kuwa yeye ni jambazi huku akidai kwamba matamshi yake yalitokana na hasira ambayo alikuwa nayo.

Alimuomba mkewe kurejea ili walee watoto wao ila Phylis kwa upande wake alimuomba ampatie muda afikirie kuhusu suala la kurejea kwake.

Phylis alimwambia Dennis amlinde mtoto wao vizuri huku akiendelea kufikiria kama atarudi kwake.