Patanisho: "Bwanangu aliniambia ataoa, alisema atakufa na wake wawili" Mwanadada asimulia masaibu ya ndoa yake

Muhtasari

•Sharon alidai kwamba ingawa bado hawajatengana ana wasiwasi kuwa huenda ndoa yao ikasambaratika kwani imekuwa ikiyumba tangu aanze kumshuku mumewe kuwa na mpango wa kando.

•Odongo alithibitisha kuwa anakadiria kuoa mke wa pili hapo baadae na kudai kuwa tayari walikuwa wamezungumzia suala hilo na mkewe.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Sharon Atieno (24) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Evans Odongo (35).

Mkazi huyo wa Nakuru alieleza kuwa amekuwa kwa ndoa na Odongo kwa kipindi cha miaka tisa na tayari wamebarikiwa na watoto wanne pamoja.

Sharon alidai kwamba ingawa bado hawajatengana ana wasiwasi kuwa huenda ndoa yao ikasambaratika kwani imekuwa ikiyumba tangu aanze kumshuku mumewe kuwa na mpango wa kando.

"Tulikuwa tunagombana tu. Alikuwa Pokot akakuja siku ya Jumamosi, tukakaa chini tukaongea. Yeye alijua tumemaliza maneno kumbe mimi bado nilikuwa na wasiwasi ndani ya roho yangu. Tulipokuwa tumelala nikachukua simu yake nikaanza kusoma jumbe kwa simu yake. Nilipata tu jumbe za kawaida tu" Sharon alisimulia.

Sharon alieleza kuwa baada ya kumaliza kupitia jumbe kwenye simu ya mumewe alimuamsha na kumueleza kuhusu kosa ambalo alikuwa ametenda ila hakuridhishwa na kitendo kile.

"Nilimuasha usiku tukaongea nikaona kama amekasirika. Aliniambia kumbe tulimaliza kuongea maneno na mimi nikaendelea kuchukua simu yake kuangalia. Nilipoona amekasirika niliita rafiki yake tukaongea.  Ilibidi sasa afungue roho yake aniambie makosa zangu zote. Hapo nikaona kweli mimi ni mtu mwenye makosa" Sharon alisimulia.

Bwana Odongo alipopigiwa simu Sharon alimuomba msamaha kwa yale yote ambayo alikuwa amemtendea huku akiapa kutorudia makosa yake.

Odongo alikubali kumsamehe mkewe  ila akakosoa sana tabia yake ya kuchukua simu yake na kuangalia jumbe zilizotumwa.

Sharon pia alifichua jambo lingine ambalo lilikuwa linampatia wasiwasi kuhusu ndoa yao. Alisema kuwa mumewe alikuwa amemwambia kuwa ana mpango wa kuoa mke wa pili.

"Aliniambia eti ataoa mwingine. Alisema ata kama hataoa saa hii eti atakufa na mabibi wawili" Sharon alisema.

Alikiri kuwa hako tayari kumpokea  mke mwenza.

Odongo alithibitisha kuwa anakadiria kuoa mke wa pili hapo baadae na kudai kuwa tayari walikuwa wamezungumzia suala hilo na mkewe.

"Mwanaume anaweza oa wanawake wale anataka. Hiyo maneno tuliongea na yeye. Mambo ni kuelewana. Hilo suala si eti huwa tunaongea saa zile niko na hasira. Huwa namwambia eti nataka kumwongezea mwanamke mwingine ili amsaidie kwa kazi za kinyumbani na kunitunza. Nikifika nyumbani kama nimechoka mwingine ananipapasa" Odongo alisema.

Hata hivo Gidi alimuonya Odongo dhidi ya kuoa mke wa pili wakati mke wake bado angali na umri mdogo kwani ni ngumu kwake kuelewa hatua hiyo.