Patanisho: Mama mkwe akataa kusamehe jamaa aliyemtusi kahaba na kupiga bintiye mbele yake

Muhtasari

•Mjomba alidai kuwa bibi yake alinyakuliwa na jamaa mwingine akaenda na watoto wawili na kumuachia watoto wanne.

•Mama Phylis alifichua kuwa Mjomba ana mazoea ya kumpiga mkewe na isitoshe huwa hazingatii heshima kila anapoenda kumshawishi arudi.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama David Mjomba (33) kutoka Taita Taveta alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Phylis Majala (25) ambaye walikosana na mwezi mmoja uliopita.

Mjomba alisema kwamba amekuwa kwa ndoa na Phylis kwa zaidi ya mwongo mmoja na katika kipindi hicho wamebarikiwa na watoto sita.

Mjomba alidai kuwa bibi yake alinyakuliwa na jamaa mwingine akaenda na watoto wawili na kumuachia watoto wanne.

Licha ya kushtumu mkewe kujihusisha na mipango wa kando Mjomba alidai kwamba angali anampenda sana na angetamani warejeane.

Alisema kuwa juhudi zake za kujaribu kurejesha mkewe zimekuwa zikigonga mwamba kwani kila anapoenda kwao mama mkwe huwa mkali kwake na kumpa vitisho vikali.

Ghost alipojaribu kuwasiliana na mke wa Mjomba aliyepokea simu sio mwingine ila mama yake Phylis. Mama Phylis alisema kuwa bintiye hakuwa pale nyumbani kwa wakati ule.

Hata hivyo mama Phylis alifichua mengi ambayo Mjomba hakuwa ameeleza hapo awali. Alimtaja Mjomba kuwa mwenye vurugu na asiye na maadili.

Mama Phylis alifichua kuwa Mjomba ana mazoea ya kumpiga mkewe na isitoshe huwa hazingatii heshima kila anapoenda kumshawishi arudi.

"Anaogopa kitu gani? Yeye akija huwa na matusi. Huwa ananiita mimi Malaya. Alikuja akapiga msichana wangu hapa nyumbani. Alisema eti nilimfunza umalaya kwani nafanya umalaya. Nilimuuliza ama tunafanya umalaya na yeye. Alimpiga binti yangu hapa nje kwangu. Niliona amempiga hata mimi nikampiga kofi. Amezoea kuja na matusi na kuniita Malaya" Mama Phylis alisema.

Mama Phylis alisema kwamba bintiye alilazimika kuenda mafichoni kwa mamake mkubwa kwani Mjomba alikuwa anamwandama sana akidai kuchukua mtoto wake wa kike.

Mama Phylis alikataa kumsamehe Mjomba huku akimshauri atafute namna ya kutafuta kikao wajadiliane watakavyosuluhisha mzozo wao.

"Utasamehewa saa hii alafu kesho unarudia hayo maneno.. Yule bibi ulisema utaleta umwambie aje alee watoto" Mama Phylis aliambia Mjomba.

Mjomba alisema kwamba watoto wanne alioachiwa na mkewe walikuwa wanateseka wakidai mama yao arejee.

"Arudi nyumbani alee watoto. Saa hii wanateseka hapa nyumbani. Kwanza hawa wawili wadogo wanaenda shuleni hawali, tena nyumbani hawali wanakataa kukula kwa sababu wanataka mama yao" Mjomba alisema. 

Ghost alimshauri Mjomba atafute wazee waandamane nao hadi kwa kina Phylis ili wajaribu kusuluhisha mzozo uliokuwepo.