"Aliniambia machozi ambayo alilia itanisumbua" Jamaa adai aliyekuwa mpenziwe alimfunga baada ya kugundua ameoa mke mwingine

Muhtasari

•Nathan alisema  walikosana na Jackline mwezi Agosti baada yake kugundua kwamba alikuwa amefunga ndoa na mwanamke mwingine.

•Nathan alisema anashuku Jackline  alimwendea kwa mganga kwani tangu alipomwambia machozi aliyomwaga yangeathiri maisha yake hali haijakuwa nzuri.

•Alisema kwamba ndoa yake ya sasa haijakuwa imara kwani huwa anakorofishana na mkewe mara kwa mara.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Nathan Kiriungu (25)  kutoka Kitui alituma ujumbe akiomba kupatiwa nafasi ya kumwomba msamaha mwanadada ambaye alikuwa anachumbia, Jackline Kalumi (25).

Nathan alisema  walikosana na Jackline mwezi Agosti baada yake kugundua kwamba alikuwa amefunga ndoa na mwanamke mwingine.

Alieleza kuwa Jackline alighadhabika sana baada ya kugundua hayo na akasema maneno makali ambayo anahofia huenda ndiyo yanamsababishia masaibu yaliyomkumba kwa sasa. 

"Jackline alikuwa mpenzi wangu. Niliamua kuoa mwanamke mwingine kwa kuwa tulikuwa tumezaa na yeye. Tulikuwa tumepanga kuoana na Jackline na alipogundua nimeoa mwanamke mwingine wakakorofishana sana. Nilipojaribu kuongea na yeye aliniambia eti machozi ambayo amelia itanisumbua. Nilioana ni kama alinilaani. Saa hii ni kama inanisumbua sababu sioni maisha yangu yakiendelea vizuri" Nathan alisimulia.

Nathan alisema anashuku Jackline alimwendea kwa mganga kwani tangu alipomwambia machozi aliyomwaga yangeathiri maisha yake hali haijakuwa nzuri.

Alisema kwamba ndoa yake ya sasa haijakuwa imara kwani huwa anakorofishana na mkewe mara kwa mara.

"Alikuwa amepeleka mtoto shule na akamwandikisha na jina langu. Aliniuliza ingekuwaje sasa kwa kuwa tayari alikuwa amemwandikisha kwa jina langu. Nilimwambia sikuwa na lingine la kufanya kwa kuwa nilikuwa nimeoa mwanamke mwingine.Akaniambia machozi yake itanisumbua. Huyo mtoto si wangu nilimpata akiwa na yeye. Aliniambia eti alilia usiku mzima" Nathan alisema.

Nathan alidhirisha kwamba nia yake kuomba msamaha ni kwa sababu alitaka kufunguliwa mambo yake iache kuharibika wala sio eti alitaka warudiane.

Juhudi za kuwasiliana na Jackline ili waweze kupatana na Nathan hata hivyo hazikufua dafu kwani alisita kuchukua simu licha ya kupigiwa mara tatu.

Nathan alipopatiwa nafasi ya kumuomba Jackline msamaha hewani alilemewa na kuishiwa na maneno kisha akakata simu.