Patanisho: Jamaa adanganya mkewe mjamzito arudi kwao akiahidi kumuendea kisha aoa mwingine

Muhtasari

•Mwanadada huyo aliporudi kwa mumewe kufuatilia kilichokuwa kinaendelea aligundua kuwa mwanamke mwingine tayari alikuwa amechukua nafasi yake pale.

•Dan alipopigiwa simu alimruka Linet huku akidai kwamba hawakuwahi kuwa pamoja kwenye ndoa ila wao marafiki tu.

Gidi na Ghost asubuhi
Gidi na Ghost asubuhi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada alliyejitambulisha kama Linet Kadogo alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Dan ambaye walitengana mwaka jana.

Linet alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilivunjika mnamo mwezi Machi mwaka jana wakati mumewe alimshawishi aende atulie nyumbani kwao kwa kipindi kifupi akiahidi kumuendea baada ya siku chache ili wapange ndoa ila siku nyingi zikapita bila kusikia lolote kutoka kwake.

Mwanadada huyo aliporudi kwa mumewe kufuatilia kilichokuwa kinaendelea aligundua kuwa mwanamke mwingine tayari alikuwa amechukua nafasi yake pale.

"Aliponiambia niende nijitayarishe anakuja kunioa nilitoka nikaenda nyumbani kwetu. Nikakaa wiki ya kwanza ikaisha, tulikuwa tunaongea ndio lakini alikuwa ananiambia tu eti wanakuja. Ya pili ikaisha, ya tatu vilevile. Nikadhani labda hakuwa amejipanga. Nilipouliza aliniambia kuwa ndugu yake ameumia mgongo baada ya kupata ajali eti nisubiri apone ili wakuje. 

Mamangu aliniambia nirudi kwa sababu nilikuwa mjamzito. Aliporudi kutoka kazini aliniuliza mbona nilirudi bila kumwarifu, nikamweleza. Baada ya siku mbili akaleta mwanamke mwingine akasema tukae sote wawili. Mimi nilibakia pale yule mwanamke alienda baada ya kugundua mimi ni bibi ya jamaa huyo. Tukakaa na mume wangu lakini baada ya wiki mbili akaanza kupanga manguo eti anaenda. Hatuishi pamoja, nilitoka huko mwezi wa sita" Linet alieleza

Linet alisema baada ya kutoka kwa mumewe alirudi nyumbani kwao ila wazazi wake hawakumtaka pale. Alisema hata baada ya kujifungua mumewe alikataa kushugulikia mtoto wao.

Dan alipopigiwa simu alimruka Linet huku akidai kwamba hawakuwahi kuwa pamoja kwenye ndoa ila wao marafiki tu. Alimshtumu Linet kwa kulazimisha ndoa.

"Huyo si mke wangu, amekuwa rafiki. Yeye ndiye anataka nimuoe. Hajawahi kuwa mke wangu" Alisema.

Linet alisistiza kuwa Dan ni mume wake na hata yeye ndiye aliyempatia  mtoto wao jina. 

Wawili hao hawakuweza kupatana kwani Dan alikataa kuzungumza tena na Linet na akakata simu yetu.