Patanisho: "Aliniambia mtoto sio wangu, ako na babake polisi"

Muhtasari

•Caroline alisema ndoa yake ya miaka saba ilivunjika baada ya mumewe kumshutumu kwa kuenda nje ya ndoa.

•Peter alimshtumu mkewe kwa kukosa kuheshimu ndoa yao na kupenda kuponda raha huku akiapa kuwa kamwe hawezi kurudiana naye.

•Caroline alikata simu wakati Peter alikuwa anaendelea kutoboa maovu kumhusu na alipotafutwa kwa mara nyingine tayari alikuwa ameizima.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Caroline Naliaka ,31, kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Peter Shikuku ambaye walikosana mnamo mwezi Mei mwaka jana.

Caroline alisema ndoa yake ya miaka saba ilivunjika baada ya mumewe kumshutumu kwa kuenda nje ya ndoa.

Alisema mumuwe alichochewa dhidi yake na majirani ambao walimshutumu kwa kosa la uasherati wakati alikuwa ameenda kazi mbali na nyumbani hayupo.

"Aliniponioa alikuwa na mke lakini walikuwa wameachana  na akaachiwa watoto watatu. Nilikaa na watoto hao huo muda wote hadi tukabarikiwa na mtoto mmoja naye. Baadae alipata kazi nje na akaniacha nao kwa nyumba. Alienda akakaa miezi sita bila kurudi. Alirudi na kisirani akaniambia eti amepata habari kuwa naenda nje ya ndoa. Ni mtu ambaye huwa anatumiapombe, alichukua panga akatishia kunikatakata. Jirani ndiye aliniokoa. Nilichukua mtoto nikarudi kwetu" Caroline 

Caroline alifichua kuwa wamekuwa wakizungumza na Peter katika juhudi za kurudiana ila bado hakujakuwepo na mpango mzuri.

Peter alipopigiwa simu aligeuza hadithi dhidi ya mkewe na kwa uchungu mwingi akafichua mengi maovu kumhusu.

Alimshtumu mkewe kwa kukosa kuheshimu ndoa yao na kupenda kuponda raha huku akiapa kuwa kamwe hawezi kurudiana naye. Hali kadhalika alisema kuwa Caroline aliwahi kumfichulia kuwa mtoto mmoja aliyedhani kuwa ni wake sio wake.

"Alifukuzwa kwa boma yake ya kwanza. Tena akakuja kuendeleza tabia zake mbaya. Mimi naenda kazi yeye anafungia watoto kwa nyumba anaenda kucheza. Alikuwa analeta wanaume kwa nyumba yangu. Apambane na maisha yake aachane na mimi, siwezi kubali kurudisha kwangu.. Ako na tabia mbaya, mwanamke akiolewa anafaa kujua nyumba ni yangu, sio mambo ya kuleta wanaume na kuacha watoto kwa nyumba na kuenda kucheza. Arudi mahali alikuwa ameoleka, mimi simtaki.

Tena yeye alisema kwetu huwa tunaua watu, anarudi kufanya nini basi? Anataka kurudi mimi nimuue. Mimi niko na watoto wangu watatu, wako kwangu. Mimi sikupata mtoto, alisema mtoto ako na baba yake ambaye ni polisi. Huyo si mtoto wangu. Niliadhibu watoto akaenda kunishtaki. Aliniambia mtoto sio wangu" Peter alisema.

Caroline alikata simu wakati Peter alikuwa anaendelea kutoboa maovu kumhusu na alipotafutwa kwa mara nyingine tayari alikuwa ameizima.

Peter aliapa kwamba hawezi kufanya kosa la kumrudisha tena kwake kwani tayari walikuwa wamerudiana mara mbili hapo awali na makosa yakajirudia.