Patanisho: Jamaa afurushwa nyumbani na mkewe baada ya kupoteza ajira

Muhtasari

•Mulii alisema ndoa yao ya miaka mitano ilianza kusambaratika mnamo Machi 2020 wakati ambapo alipoteza kazi yake kutokana na janga la Corona.

•Peter alidai kwamba aliogopa kurudi kwa mkewe kwa kuwa alipokea vitisho kutoka kwa mwanajeshi akionywa dhidi ya kumkaribia.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi, kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Peter Mulii (37) kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Maureen Asambu (31) ambaye walitengana takriban miaka miwili iliyopita kufuatia mizozo ya kinyumbani.

Mulii alisema ndoa yao ya miaka mitano ilianza kusambaratika mnamo Machi 2020 wakati ambapo alipoteza kazi yake kutokana na janga la Corona.

Alieleza kwamba alipopoteza kazi yake mkewe alianza madharau nyumbani hadi akashinikizwa kuondoka pale na kurudi kijijini kwao.

"Nilikosa ajira kwa sababu ya Corona. Akaanza madharau kidogo kidogo, mara hafungui nyumba. Yeye ndiye alikuwa na kazi.Wakati mwingine ilikuwa inabidi nimeomba malazi kwa marafiki zangu. Baada ya miezi mitatu nilianza kuona imekuwa shida. Ilibidi nimeondoka pale nikarudi nyumbani. Baada ya Corona kuisha nilirudi mjini kufanya shughuli zingine" Peter alisema.

Peter alidai kwamba aliogopa kurudi kwa mkewe kwa kuwa alipokea vitisho kutoka kwa mwanajeshi akionywa dhidi ya kumkaribia.

"Niliona badala ya nipoteze maisha yangu hii Nairobi nikajipa shughuli nikaenda eneo lingine" Alisema.

Peter alisisitiza kwamba hapo awali hakukuwahi tokea ugomvi mwingine mkubwa kati yake na mkewe na waliishi kwa amani.

Alisema angependa uhusiano mwema urejee kati yao na waanze kuwasiliana tena huku akieleza kwamba tayari amepata kazi nyingine.

"Sikutaka mambo mingi. Nilitaka ile uhusiano mwema. Kuacha na uhusiano mwema ni vizuri. Napenda kuishi na watu vizuri. Hata  simu zangu huwa hashiki. Nilitaka nimwambie kwamba sina ubaya, sio lazima turudiane" Peter alisema.

Maureen alipopigiwa simu hata hivyo aliikata mara moja baada ya kutajiwa jina la aliyekuwa mumewe.

Peter alifichua kwamba amewahi kupata fununu kwamba Maureen tayari yuko kwenye mahusiano na mwanaume mwingine.

Je, maoni yako ni yepi kuhusu Patanisho ya leo?