"Alikuwa anasema nikae wiki mbili bila kusoma katiba!" Jamaa alalamika kunyimwa haki za ndoa na mkewe

Muhtasari

•Kemunto alisema ndoa yao ya miaka minne ilisambaratika mnamo mwaka wa 2020 baada ya mumewe kumshinikiza wapate mtoto mwingine, jambo ambalo hakukubaliana nalo.

•Michael alifichua kwamba walipokuwa katika mahusiano Kemunto alikuwa anamnyima haki zake za ndoa

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Kemunto alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Michael ambaye alisema walitengana miaka miwili iliyopita kufuatia kutoelewana nyumbani.

Kemunto alisema ndoa yao ya miaka minne ilisambaratika mnamo mwaka wa 2020 baada ya mumewe kumshinikiza wapate mtoto mwingine, jambo ambalo hakukubaliana nalo.

Alieleza kwamba baada yake kukataa kuongeza mtoto mwingine, mume wake alileta mwanamke mwingine na kudai alitaka wapate mtoto naye.

"Bwanangu aliniambia tuongeze mtoto mwingine nikakataa. Kutoka hapo akaleta mwanamke mwingine kwa nyumba akaniambia kwa kuwa nimekataa angetaka wapate naye. Nilikasirika nikamwambia tungekaa chini tuzungumze tuelewane. Alikataa akaniambia kama sitaki angetaka kupata na huyo mwingine. Nilikasirika nikatoka huko nikamwachia boma wapate na huyo mwingine" Kemunto alisimulia.

Kemunto alieleza kwamba alikataa ombi la mumewe la kuongeza mtoto kwani alihisi ilikuwa mapema sana bado na hakuwa tayari.

Alikiri kwamba alikuwa amepanga uzazi wapate mtoto wa tatu baada ya miaka saba ila mumewe hakukubaliana na suala hilo.

"Nilikuwa namweleza lakini hakuwa anataka kusikia. Alisema eti nataka azeeke haraka akufe kama hajaona watoto. Ningependa kurudi, nampigia simu ananiambia anaendelea kufikiria, sijui anafikiria hadi lini. Anashughulikia mtoto kidogo kidogo tu" Alisema.

Michael alipopigiwa simu alisema kitendo cha Kemunto kupanga uzazi miaka mingi kilimkasirisha akaamua kuleta mke mwingine.

Pia alifichua kwamba walipokuwa katika mahusiano Kemunto alikuwa anamnyima haki zake za ndoa

"Niliwahi kumwambia tujaribu tupate mtoto mvulana akakataa. Mtoto wa kwanza ni msichana, mara ya pili alienda akapanga uzazi miaka kumi na miwili. Nilioa bibi mwingine lakini pia yeye tuliachana, sina bibi. Huyo akifika huko anaanza fitina, hatakangi nisome katiba yake. Anasema nikae wiki mbili bila kusoma katiba. Nimesoma katiba miaka miwili tu" Michael alilalamika.

Kemunto aliahidi kubadilisha mienendo yake katika ndoa iwapo Michael angekubali kumchukua tena kama mke.

Michael alikubali kumsamehe Kemunto na kurudiana naye ila akamsihi abadilike ili waweze kuishi pamoja kwa amani.