Shambulio la Israel nchini Iran: Bei ya mafuta yapanda

Bei ya mafuta na dhahabu duniani zimepanda huku hisa zikishuka baada ya Marekani kusema kombora la Israel liliipiga Iran.

Muhtasari

•Wawekezaji wamekuwa wakifuatilia kwa karibu majibu ya Israel kwa shambulio la ndege zisizo na rubani na kombora la Iran wikendi iliyopita.

Image: BBC

Bei ya mafuta yapanda

Bei ya mafuta na dhahabu duniani zapanda huku hisa zikishuka baada ya maafisa wa Marekani kusema kuwa kombora la Israel liliipiga Iran.

Katika biashara ya bara Asia siku ya Ijumaa asubuhi, Mafuta ghafi yameripotiwa kupanda kwa zaidi ya 3% hadi karibu $90 kwa pipa, huku dhahabu ikiuzwa kwa bei ya juu Zaidi ya hadi $2,400 .

Masoko ya hisa ya Japan, Hong Kong na Korea Kusini pia yalianguka baada ya ripoti hizo.

Wawekezaji wamekuwa wakifuatilia kwa karibu majibu ya Israel kwa shambulio la ndege zisizo na rubani na kombora la Iran wikendi iliyopita.

Ving'ora vyasikika kaskazini mwa Israeli - kijeshi

Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa ving'ora vimelia kaskazini mwa Israel, likinukuu jeshi la Israel.

Hakuna maelezo zaidi kwa sasa na jeshi la Israel linasema halitoi maoni "kwa wakati huu".

Mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran ipo tayari kukabiliana na mashambulio - vyombo vya habari vya serikali

Shirika la habari la serikali IRNA linaripoti kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi imewekwa tayari katika majimbo kadhaa.

IRNA ilisema kuwa nchi hiyo imefungua "betri zake za ulinzi wa anga".

Waziri wa mambo ya nje wa Iran aonya kuhusu jibu la 'haraka' kwa shambulio lolote la Israel

Katika masaa yaliyotangulia ripoti za leo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alionya kwamba jibu la nchi yake kwa kulipiza kisasi kwa Israeli litakuwa "mara moja na kwa kiwango cha juu".

Alitoa maoni hayo wakati wa mahojiano kwenye CNN siku ya Alhamisi.

Mapema wiki hii, alisema mashambulizi ya nchi yake dhidi ya Israel siku ya Jumamosi - ambayo yalihusisha zaidi ya ndege zisizo na rubani 300 na makombora - yalifikia "kutumia haki ya ulinzi halali".

Tehran imeshikilia kuwa hatua iliyochukua ni kulipiza kisasi kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni shambulio la anga la Israel kwenye ubalozi wake mdogo nchini Syria tarehe 1 Aprili, ambapo watu 13 waliuawa.