Jamaa mmoja kwa jina Daniel kutoka kaunti ya Bungoma aliwasilisha ombi lake kwa Gidi na Ghost asubuhi ya Ijumaa akitaka kupatanishwa na mke wake Eunice.
Daniel alielezea kwamba mke wake alitoroka nyumbani pasi na kuwa na ugomvi wowote na alirudi kutoka kazini akapata mke hayuko nyumbani.
“Ilikuwa tarehe 20 mwezi huu nilitoka kazi nikapata mke ameondoka. Kupiga simu nyumbani mamake akashika na kuniambia kuwa alipata habari kwa majirani kuwa namtesa,” Daniel alisema.
Hata hivyo, yeye alishikilia kwamba hajawahi mtesa mke wake na Eunice alimpigia simu juzi akimwambia kwamba hakuwahi mkosea lakini akamtaka kufanya uamuzi wa kuhamia sehemu nyingine kama anamtaka arudi.
“Juzi ndio akanipigia akasema sijawahi mkosea akasema tutoke huko tuishi pahali tofauti. Yuko Bungoma kwao. Nataka tu aniambie ukweli kama atarudi ama hapana. Tumeonana tu mwaka jana,” Daniel alilia.
Hata hivyo, Gidi alimshuku Daniel kuwa huenda si mkweli, akihisi kwamba yake ni hadithi ya kubuni tu.
Watangazaji walipojaribu kumpigia Eunice, simu yake ilikosa kuingia, ikisema kwamba namba kama hiyo haipo katika matumizi kabisa.