Ronny Korir ,29, kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Mercy Cherotich ,27, ambaye alikosana naye mwaka wa 2017.
Korir alieleza kuwa mkewe alimtema baada ya kumlipia karo ya chuo kikuu kwa miaka minne.
Alisema walipatana na Mercy mwaka wa 2013 ambapo alikubali kumsomesha hadi wamalize kabla ya kuanzisha familia.
"Sababu ya kuachana haikuonekana. Ni vile alikuwa mbali, alikuwa Machakos University. Sijui aliamua aje mpaka tukaachana hivyo 2017. Baadaye mimi niliamua kutafuta bibi mwingine ikashindikana ikawa hatuelewani.Nikiwa na mrembo yeyote nafikiria yeye, kila wakati nawaza tu yeye," Korir alisema.
Alieleza kuwa tayari alikuwa amefanya harusi ya kitamaduni na Mercy ila bado hawakuwa wamejaliwa mtoto.
"Tulipatana tukapendana akaniambia kama niko serious nimsaidie. Tulianza mapenzi kidogo kisha akanitambulisha kwao na mimi nikamtambulisha kwetu. Wakati akisoma alikuwa anakuja nyumbani mpaka mwaka wa mwisho. Nilikuwa namlipia karo, ni muhula wa mwisho tu ambao sikulipa chochote," alisema.
Alifichua kuwa baada ya kutengana, mpenzi huyo wake wa zamani alijitosa kwenye mahusiano na jamaa mwingine ila wakatengana baadaye.
"Alipata mwingine sijui wakaachana. Akanitafuta akaniambia tusameheana nikamwambia itabidi tukutane na wazee. Sijawahi kumwambia turudiane kwa sababu alikuwa amenikosea zaidi. Tulikuwa tumefunga ndoa ya kienyeji na yeye. Ikikoshindikana kurudiana na yeye, naomba anifungue," alisema Korir.
Kwa bahati mbaya, Patanisho hiyo iligonga mwamba kwani Mercy alizima simu mara baada ya kusikia jina Korir.
Kufuatia hayo, Korir alisema, "Mahali ako tu afanye tu aniachilie nikipata mwingi niweze kuendelea na maisha yangu..Mercy Cherotich mimi sikuwa na ubaya na wewe. Naomba msamaha. Naomba unifungue na roho moja. Uniachilie tu na mimi nikuachilie ili maisha yetu yawe mazuri."
Je, uko na ushauri gani kwa Korir?