Jamaa aliyejitambulisha kama Eliud Wanyama ,23, kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Celine Wafula ,26, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.
Wanyama alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika Aprili mwaka huu baada ya mkewe kuenda matanga ya nyanya yake na hajawahi kurudi miezi minane baadaye.
"Nikimuuliza ananiambia nikuwe mpole. Bado sijaongea na watu wa kwao. Nilienda huko lakini sikufika kwao kwenyewe. Ilikuwa late na sikutaka nifike huko usiku. Nilikuwa na pikipiki lakini ilikuwa inasumbua kwa njia nikafika kuchelewa.
"Nilitaka kujua msimamo wake ili nijue jinsi nitajipanga. Anasema tu nikuwe mpole ako tu," Wanyama alisema.
Celine alikana kumfahamu Wanyama na kudokeza kuwa yeye ni Mkamba na si Mluhya kama jamaa huyo alivyodai.
"Ati hunijui! Miezi saba tayari umenisahau? Wewe si ni Celine, bibi wa kwangu," Wanyama alijibu baada ya mwanadada huyo kumkana.
Celine alimjibu, "Ati bibi wa kwako? Mimi hata sijawahi kuoleka na sijafikisha miaka ya kuoleka. Hata Sijafikisha miaka 26, labda umekosea numba. Mimi bado nasoma. Mimi ni Mkamba, nimetoka Ukambani."
Aliongeza, "Mimi ni Mkamba, saa hii niko holiday. Mimi mwenyewe sikujui. Ati Wanyama, mimi sijawahi kuskia jina hilo."
Wanyama alisisitiza kuwa mwanadada aliyekuwa akizungumza upande mwingine wa simu ni mkewe na kudai wamekuwa wakiongea.
Mwanadada huyo hata hivyo alisisitiza kuwa ingawa jina lake halisi ni Celine, yeye hajawahi kuolewa na Wanyama.
"Hii ni kama imeenda kabisa!" Wanyama alisema kabla ya Gidi kumaliza Patanisho.
Gidi alibainisha kwamba wawili hao hawakueleweka na kudokeza huenda walikuwa wakicheza tu.
"Bure kabisa!" alisema.
Je, maoni yako ni yepi kuhusu Patanisho ya leo?