Jamaa kwa jina Dennis Arasa Minogo ,27, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Ann Munaniye ,24, ambaye alimuacha wiki chache zilizopita.
Dennis alisema mkewe aligura ndoa yao ya takriban miaka miwili unusu baada ya wao kugombana kidogo takriban tatu zilizopita.
Alisema mkewe alikuwa akimshtumu kwa kuwa na mipango wa kando, jambo ambalo alipinga.
"Mke wangu amekuwa akinishuku. Nikitoka anadhani naenda kutafuta wanawake. Mimi humwambia natoka kumtafutia kwa kuwa ile kazi nilikuwa nafanya iliisha. Kuna siku niliugua usiku, nikaenda hospitali nikaandikiwa sindano nyingi. Jumamosi fulani nilimwambia naenda kumalizia sindano niliandikiwa. Kurudi nilipata hayuko ameenda. Simu yake aliiacha hapa, lakini imeharibika kidogo ndio maana ameiacha," Dennis alisema.
Juhudi za kumpata Bi Ann hazikufua dafu. Hata hivyo, mamake Ann alishika simu na kueleza kwamba bintiye hakutaka kuongea naye.
Zaidi, mamake Ann alieleza kwamba bintiye alimwambia mzazi huyo mwenzake alikuwa akimtesa sana. Pia alifichua kwamba Dennis hajawahi kujitambulisha kwao
"Ananiambia anamtesa sana. Bado hajajitambulisha kwetu. Tunaongea na mtu na hatujamjua. Hajafika huku kwetu. Amekaa naye miaka miwili!" Mamake Ann alisema.
Huku akijitetea, Dennis alisema, "Tulikuwa tumepanga tunaenda mwezi wa kwanza.Msichana alikuwa na mimba. Nikaona haitawezekana kuenda kwao akiwa na mimba
Mamake Ann alisema, "Baba yake atajibu kama atarudi. Kwa sasa aache atulie kwanza. Dennis aache Ann apumzike, atulize akili. Ako na mtoto wake."
"Huyo Dennis simjui na ni mzazi mwenza wa Ann. Amekaa na mtoto wangu miaka miwili. Sikujua mtoto ako wapi. Nilifanya juu chini nikamtafutia nauli akuje. Niko na uchungu sana, anadhani mtoto ni wa bure," aliongeza.
Je, ushauri wako ama maoni kuhusu Patanisho ya leo ni yapi?