Mwanamuziki Guardian Angel na mkewe Esther Musila wamefichua walichumbiana kwa chini ya mwezi mmoja tu kabla ya kutulia pamoja kwenye mahusiano.
Wakiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni katika kitengo cha Ilikuaje, wanandoa hao walifichua kwamba tayari walikuwa wamependana ndani ya mwezi wa kwanza baada ya kukutana.
Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza mnamo Machi 13, 2020 kupitia usaidizi wa mtangazaji Maina Kageni.
"Haikuchukua mwezi... Katika mwezi wa kwanza tulikuwa tumependana," Guardian Angel alisema.
Mwanamuziki huyo mwenye umri miaka 35 alikiri kuwa alimpenda mkewe punde walipokutana kwa mara ya kwanza.
Bi Musila, 52, ndiye aliyependekeza kukutana na msanii huyo baada ya kufurahishwa na wimbo wake mmoja aliousikia redioni. Hata hivyo aliweka wazi kuwa nia yake haikuwa kuchumbiana naye.
"Mimi na Maina tulifanya kumtengeneza msanii huyu. Tumpatie anachofaa. Huo ndio ulikuwa mpango wangu. Lazima angejulikana zaidi," Alisema.
Mama huyo wa watoto watatu alifichua kuwa Guardian Angel alimualika wiki mbili baada ya kukutana na hapo ndipo alipiga hatua ya kufungua moyo wake.
Musila alisema kwamba hata hivyo alisitasita kuhusu uhusiano huo kwani alihofia watu wangesema nini.
"Nilikuwa natoka kwa maisha ya faragha na kuingia maisha ya umaarufu, umri wangu ndio ulikuwa shida. Shida yangu ilikuwa watu wangesema nini, sio hata familia yangu ingesema nini," Musila alisema.
Guardian Angel kwa upande wake aliweka wazi kuwa hakuwahi kuwa na shida na pengo kubwa kati ya umri wao.
Musila alifichua kuwa baada yao kukubaliana kuhusu mahusiano aligura kwake na kuhamia kwa mwanamuziki huyo.
"Nilihama. Bado niko na kwangu kwa sababu watoto wangu bado wanaishi pale lakini nilipanga nusu ya nguo zangu na kuhamia kwake," Musila alisema.
Wawili hao walifunga pingu za maisha Januari mwaka huu na wameendelea kufurahia ndoa yao licha ya kejeli nyingi hasa kwenye mitandao ya kijamii.