In Summary

•Muthoni alidai kwamba mzazi mwenzake Mulamwah alizichukua akaunti zake  baada yao kutofautiana kuzihusu na amekuwa akizisimamia tangu wakati huo.

•Alisisitiza kuwa Mulamwah ndiye baba mzazi wa bintiye Keilah Oyando  na kudai kwamba hata wanafanana kwa sura.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu kama Carrol Sonnie amemshtumu  mpenzi wake wa zamani mchekeshaji Mulamwah kwa kuchukua akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Akiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, mama huyo wa mtoto mmoja alifichua kwamba hazimiliki tena akaunti zake za Instagram na Facebook (Carrol_Sonnie)  ambazo zilikuwa zimejizolea ufuasi mkubwa tayari.

Muthoni alidai kwamba mzazi mwenzake Mulamwah alizichukua akaunti zake  baada yao kutofautiana kuzihusu na amekuwa akizisimamia tangu wakati huo.

"Sina akaunti hizo, sizisimamii wala kuziendeleza. Niliamua kuanza upya, niliona ni vizuri nikubali kulivyoenda. Ni wakati wa kusonga mbele. Mimi na mpenzi wangu wa zamani tulitofautiana kuhusu akaunti hizo. Sipendi kushinda nimevutana" Muthoni alisema.

Mwigizaji huyo alifichua kwamba kuna mengi ambayo yalipelekea hatua hiyo ila akasita kumwaya mtama wote huku akieleza kuwa bado hayuko sawa kabisa kuzungumza.

Alisema kwamba tayari amefungua akaunti mpya za ambazo anazisimamia yeye mwenyewe bila kuingiliwa na baba ya bintiye. 

"Niliamua kutengeneza akaunti zangu upya, zinaitwa Carrol_Muthoni.. Sasa situmii jina Sonnie" Mwigizaji huyo alisema.

Muthoni pia alisisitiza kuwa Mulamwah ndiye baba mzazi wa bintiye Keilah Oyando na kudai kwamba hata wanafanana kwa sura.

View Comments