In Summary

• Khalwale alifichua kwamba mtoto huyo alizaliwa Jumatatu usiku katika hospitali ya Nairobi.

Dkt. Boni Khalwale Aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale akifurahikia ujio wa mjukuu wake
Image: Twitter

Familia ya aliyekuwa seneta wa kwanza wa Kakamega, Dkt. Boni Khalwale ni moja kati ya familia zisizoishiwa na furaha, si tu kutokana na ubora wa maisha bali pia kutokana na baraka wanazomiminiwa na Mwenyezi Mungu.

Kwa mara nyingine tena, familia hiyo inasherehekea ujio wa mwanao mchanga ambaye alizaliwa Jumatatu usiku wiki hii.

Akisherehekea zawadi hii mpya katika familia yake, mwanasiasa huyo alipeleka kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuwataarifu wafuasi wake kwamba familia yake imempokea mtoto mwingine tena aliyezaliwa katika hospitali ya Nairobi.

Khalwale alimsifia mwanawe Tigana Khalwale kwa kumpatia mjukuu ambaye alisema amejaza kikamilifu pengo lililoachwa na marehemu mkewe, Adelaide Shikanga Khalwale.

“Baraka kwa wingi. Jana usiku katika Hospitali ya Nairobi, kusubiri kwa muda mrefu kuzaliwa upya kwa mke wangu marehemu Adelaide Shikanga Khalwale kulifikia mwisho wa furaha. Mungu aliibariki familia yangu na CANDICE SHIKANGA KHALWALE. Hongera sana @TKhalwale kwa ajili ya kuziba pengo lililoachwa na kifo cha mama yako,” aliandika Khalwale kwa furaha.

Mheshimiwa Khalwale amekuwa akigonga vichwa vya habari kila mwaka haswa matokeo ya mitihani ya kitaifa yanapotangazwa na Waziri wa elimu kutokana na dhana kwamba yeye kwa miaka ya hivi karibuni amekuwa akisherehekea mmoja kati ya wanafamilia wake kufuzu katika mitihani hiyo.

Watu wengi wamekuwa wakisema kwamba kama vile ubashiri, kila mwaka lazima mheshimiwa Khalwale awe na mtahiniwa katika mitihani ya kitaifa, iwe darasa la nane au kidato cha nne, na bila shaka ujio wa mjukuu wake ni ongezeko jingine katika familia yake ambapo kutampa nafasi mwanasiasa huyo kuzidi kusherehekea mafanikio ya wanafamilia yake katika miaka ijayo.

Khalwale analenga kurudi kwenye seneti tena katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kupitia tikiti ya chama cha UDA, ambapo awali alikuwa analenga kuwa gavana wa Kakamega lakini baada ya mazungumzo ya kina alitangaza kumuunga mkono seneta wa sasa Cleophas Malala kuwania ugavana na yeye akaamua kurudi tena katika kinyang’anyiro cha ugavana baada ya kushindwa ugavana uchaguzi uliopita na gavana wa sasa Wycliffe Oparanya.

View Comments