In Summary

•Rayvanny alikuwa amepatiwa notisi ya faini iwapo angeonekana kwenye jukwaa yoyote kabla ya makubaliano kuafikiwa.

•Rayvanny anaripotiwa kuikimbilia BASATA kuomba usaidizi kufuatia faini kali zilizowekwa mbele yake na WCB.

Image: INSTAGRAM// RAYVANNY

Staa wa Bongo Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny anaripotiwa kutozwa faini ya Tsh50M (Ksh2M) na lebo yake ya zamani WCB.

Ripoti kutoka Bongo zinaarifu kuwa WCB ilimtoza Rayvanny faini hiyo kwa kupanda jukwaa kwenye shoo ya Nandy.

Kulingana na mtangazaji  maarufu Mwijaku, mwanzilishi huyo wa Next Level Music alikiuka makubaliano yake na WCB kwani hakutakiwa kuonekana kwenye jukwaa yoyote kabla ya mchakato wa kuondoka kwake kukamilika.

Inadaiwa kuwa lebo hiyo inayomilikiwa na  Diamond Platnumz bado haikuwa imemwachilia huru Rayvanny wakati alipotumbuiza kwenye shoo ya Nandy kwani bado hakuwa amekamilisha malipo ya Tsh800M alizodaiwa.

"Mwanzo alipoambiwa alipe milioni 800 ili aondoke, alikubali kulipa. Lakini kukawa na mvutano kuhusu akaunti zake za mitandao ya kidijitali. Wakawa hawajamalizana bado. Yeye alisimamisha malipo ya  800M zile ili kwanza wakubaliane kuwa akilipa pesa zile zote watampa akaunti zake zote za kidijitali," Mwijaku alisema kwenye Clouds Media.

Inaripotiwa kwamba wakati Rayvanny aliibukia kwenye shoo ya Nandy  suluhu ya kuondoka kwake haikuwa imepatikana bado.

Mwijaku alidai kuwa staa huyo alikuwa amepatiwa notisi ya faini iwapo angeonekana kwenye jukwaa yoyote kabla ya makubaliano kuafikiwa.

"Wale wana utaratibu, ukienda kwenye disco/klabu ni milioni 5, ukienda kwenye tamasha la wazi 50M," Alisema Mwijaku.

Alisema kuwa msanii huyo alikimbilia BASATA kuomba usaidizi kufuatia faini kali zilizowekwa mbele yake na WCB lakini ikabainika lebo hiyo ya Diamond haijakiuka makubaliano yoyote ya mkataba.

"Aliagizwa kuonyesha barua ya kuachiliwa kuonyesha kuwa ameruhusiwa kupanda kwenye jukwaa fulani, hana! Kwa hiyo anahitajika kulipa 50M bila kujua ikiwa atapata akaunti zake za kidijitali," Alisema.

Tetesi hizo zimezua gumzo kubwa mitandaoni huku wito ukitolewa kwa wasanii kusoma na kuelewa mikataba kabla ya kutia saini na lebo yoyote.

Licha ya tetesi hizo Rayvanny mwenyewe amedokeza kuwa tayari  mchakato wa kuondoka kwa WCB umekamilika.

"Habari watu wangu. Rayvanny ni msanii huru. Wasiliana na usimamizi wangu mpya kwa bookings," Alisema kupitia Instastori zake.

Rayvanny alionyesha WCB mgongo mapema mwezi jana baada ya kuwa chini ya usimamizi wa lebo hiyo kwa miaka sita.

View Comments