In Summary

• Harmonize na Konde Gang wameshtumiwa kwa kununua 'views' kwenye mtandao wa YouTube baada ya ngoma zao kuandikisha rekodi zisizoaminika.

Harmonize, Ibraah na walinzi wa Konde Gang
Image: INSTAGRAM///HARMONIZE

Kwa muda mrefu sasa wasanii kutoka rekodi lebo ya Konde Music Worldwide wakiongozwa na kinara wao msanii Harmonize wamekuwa wakikashfishwa kwa kile baadhi ya mashabiki wanahisi kwamba lebo hiyo inaghushi idadi ya watazamaji bandia katika ngoma zao kwenye mtandao wa YouTube.

Wale wanaodai hivyo wanasema kwamba wakati mwingine idadi ya ‘views’ kwenye YouTube za wasanii hao huwa si kweli kwani mambo mengine ni nje ya uwezo hata kama ulikuwa umetafuta kiki ya kufa kwa kuwandaa mashabiki na wafuasi kuwa ange kwa kuingia na kuitizama kazi pindi tu unapoiachia, tena kwa mamilioni chini ya sekunde za kuhesabiwa tu!

Madai haya yalianza mwaka mmoja uliopita wakati msanii Harmonize aliachia collabo yenye nguvu na wasanii wakongwe H-Baba na nguli wa lingala Awilo Longomba, kibao kilichokwenda kwa jina la Attitude.

Kibao hicho kilizua mjadala mkali mitandaoni baada ya kuvunja rekodi mbalimbali ambazo baadae zilionekana kukwama tena na hivyo kuwachanganya mashabiki mpaka baadhi kuhisi kuna kitu kinaendelea na kwamba watazamaji kwenye ngoma hiyo huenda si wa kweli.

Kwa mfano, ngoma hiyo ilipotoka kabla ya video yenyewe, chini ya siku moja ngoma ilipiga watazamaji 642K ambapo baadae tena ‘views’ hizi zilionekana kushuka pakubwa ambapo zilitia nanga kwa kiwango cha 517K chini ya huo huo muda wa saa ishirini na nne.

Video nayo ikatoka na kuendeleza ndarire na miujiza ya Musa na Firauni ambayo bado maswali mengi yalibaki vichwani mwa watu na mpaka sasa hayajapata kujibiwa.

Video ya Attitude iliandikisha rekodi ya kupata ‘views’ 900K chini ya saa ishirini na nne na baadae ndani ya muda huo huo ikaporomoka hadi ‘views’ 700K.

Tukio hili la nadra sana kutokea lilizidi mpaka Harmonize mwenyewe ikabidi alizungumzie ambapo aliwataka mashabiki wake kutomlaumu mtu yeyote kwenye YouTube bali kujiburudisha tu na muziki.

Haya, mwaka mmoja baadae, matukio kama yale tena yameonekana kujirudia katika chaneli za YouTube za wasanii wa lebo hiyo ambapo wiki iliyopita, msanii Ibraah aliachia kibao kwa jina Rara ambacho pia rekodi zake zilishtua mno.

Kibao hicho cha Ibraah kilifikisha ‘views’ 312K chini ya sekunde hamsini, yaani hata kabla dakika moja kuisha tayari kibao kilikuwa katika mbio zaidi ya kiberenge juu ya reli.

Hili lilitisha mno ambapo wengi walidhani kwa kasi ile, kibao hicho kingefika watazamaji zaidi ya milioni 50 baada tu ya siku moja, lakini ajabu ni kwamba siku kumi na moja baadae, kibao hicho kimekwama na ‘views’ milioni 1.2

Kama hiyo haitoshi, Jumanne Harmonize aliachia collabo na Ibraah ambapo pia rekodi zake kwa mara nyingine zilisimamisha wapenzi wa bongo fleva.

Collabo hiyo kwa jina la Mdomo ilikimbia katika ‘views’ kushinda hata duma ambapo chini tu ya dakika 3, tayari Harmonize na Ibraah walikuwa wanajivunia ‘views’ milioni 1.3 kwenye YouTube, maajabu!

Ajabu zaidi ni kwamba ‘views’ hizo zilifika hapo zikagoma kidogo kama vile zilipata panchari na hadi dakika ya 6 bado hakuna ongezeko hala moja lililoshuhudiwa. Watu, wakashangaa!

Kufikia Jumatano mchana, takribani saa 24 tangu collabo hiyo kudondoshwa na kuonekana kufanya vizuri mno, bado ‘views’ zilikuwa zimetia nanga kwa idadi ya milioni 1.4, yaani kwa hesabu na takwimu za haraka haraka tu ni kwamba ngoma hiyo ilitengeneza ‘views’ milioni 1.3 chini ya dakika 3 na kushindwa kuongeza ‘views’ 100K kwa zaidi ya saa 10.

Kama huu si utapeli basi utakuwa ulaghai wa kimagumashi!

View Comments