In Summary

• “Bobi ni mtu jasiri anayepigana dhidi ya udikteta wa Jenerali Museveni nchini Uganda" - Mwangi.

Mwanasiasa wa upinzani wa Uganda Bobi Wine na mwanaharakati nchini Kenya, Boniface Mwangi
Image: Instagram//BonifaceMwangi

Mwanaharakati Boniface Mwangi amepakia picha ya pamoja na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine huku akimsifia pakubwa kwa ukakamavu ambao anasema ndio utaleta ukombozi nchini humo baada ya kipindi kirefu cha utawala dhalimu wa rais wa muda wote Yoweri Museveni.

Mwangi alisema Bobi ndiye sababu Uganda itapata ukombozi kwa kumung’atua mamlaka kwa lazima rais Museveni ambaye anasema ni katili ambaye anataka kufia madarakani lakini Bibi atafanikiwa kumng’oa kabla hajafia huko.

“Bobi ni mtu jasiri anayepigana dhidi ya udikteta wa Jenerali Museveni nchini Uganda. M7 anataka kufia madarakani lakini Bobi na kizazi chake watamaliza utawala katili wa Museveni. Aluta Continua...!” Boniface Mwangi aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Bobi Wine ambaye alikuwa mwanamuziki wa kizazi kipya kabla ya kujibwaga kwenye siasa ako humu nchini pamoja na viongozi wengine wa Afrika Mashariki kama vile rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete miongoni mwa wengine kama waangalizi wa kuhakikisha uchaguzi wa haki na amani huku Wakenya wakisubiria kutaarifiwa viongozi wapya baada ya kushiriki katika mchakato wa kupiga kura Jumanne.

“Ni vizuri kuona na kubarizi na kaka yangu @bobiwine ambaye yuko hapa kutazama #KenyaDecides2022. Wapiga kura wamefanya jukumu lao, na sasa ni juu ya IEBC kufanya kazi yao,” Mwangi aliandika.

Mwangi ambaye wanawiana na Wine kiharakati anampigia debe kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga licha ya kuwa mkosoaji wake mkubwa katika chaguzi za awali.

Wengi wanachanganua kwamba Mwangi aliamua kujitupa nyuma ya Raila kutokana na rafiki yake wa muda mrefu wakili Martha Karua kuteuliwa kama mgombea mwenza wa Raila katika uchaguzi ambao umefanyika Agosti 9.

View Comments