In Summary

• Hili linajiri siku chache baada ya kugura Jubilee iliyoko kwenye muungano wa Azimio na kuingia UDA ya Kenya Kwanza.

Bahati aongozana na Charlene Ruto kwenye hafla Embu.
Image: Instagram

Siku chache tu baada ya kutangaza kujiunga na chama tawala cha UDA, mwanamuziki ambaye pia ni mwanasiasa, Bahati Kioko ameanza kufanya ziara za hapa na pale na binti wa kwanza wa rais, Charlene Ruto.

Mapema wiki hii, msanii huyo alitangaza kujiunga na chama cha UDA na  baada ya kugura mrengo ule wa Azimio kufuatia mshikemshike uliotokea siku chache kuelekea uchaguzi wa Agosti mwaka jana ambapo alidokeza kunyimwa tikiti ya chama cha Jubilee.

Baada ya kuingia UDA, Ijumaa aliongozana na gavana wa kaunti ya Embu, Cecile Mbarire ambaye pia ni mwenyekiti mpya wa chama hicho pamoja na binti wa rais Ruto Charlene Ruto katika hafla moja huko Embu.

“Asubuhi ya Leo niliandamana na Binti wa Kwanza wa Rais Dada Yangu Charlene Ruto na Mheshimiwa Cecile Mbarire Gavana wa Embu na Mwenyekiti wa U.D.A Tulipohudhuria hafla ya Kuwawezesha Wanamuziki na Wasanii Wabunifu wa Kaunti ya Embu,” Bahati aliandika kweney picha ya pamoja ya wote watatu.

Msanii huyo ambaye ana azma kubwa ya kuwa rais wa Kenya katika uchaguzi wa mwaka 2037 aliwania Ubunge wa Mathare katika uchaguzi wa 2022 kwa tikiti ya chama cha Jubilee lakini akabwagwa vikali hadi nafasi ya tatu.

Bahati alipitia changamoto si haba baada ya Azimio kumtaka kufutilia mbali uwaniaji wake kwa tikiti ya Jubilee kwa kile walitaka Jubilee kumuunga mkono mwaniaji wa UDA, ambaye pia ni mbunge wa eneo hilo aliyelenga kutetea wadhifa wake, Anthony Oluoch.

Mwanzo alidai kupewa tikiti ya Jubilee na baadae akanyanganywa na kisha kuirudishiwa tena baada ya kuonekana kwenye vyombo vya habari akilia kwikwi na kutiririkwa na machozi.

Debeni, Oluoch wa ODM aliibuka mshindi huku nafasi ya pili ikichukuliwa na UDA na Bahati wa Jubilee akashika nafasi ya tatu kwa kura elfu 8 na ushee tu!

View Comments