In Summary

• "Nifundishe kuwa na furaha siku zote, kuomba bila kukoma, na kushukuru katika hali zangu zote.” - Fatxo.

DJ Fatxo amwaga machozi kanisani akiombewa.
Image: Screengrab.. Instagram

Wiki moja baada ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kufikisha umri wa miaka 27, mcheza santuri na msanii wa Mugithi DJ Fatxo Jumapili iliyopita alikuwa kanisani kutafuta Baraka.

Katika video ambayo msanii huyo aliipakia kwenye ukurasa wake wa Facebook na Instagram, alionekana akiwa amepiga magoti na kusujudu pamoja na wengine kwenye madhabahu mbele ya mchungaji katika kanisa moja jijini Nairobi.

Baada ya kuombewa, Fatxo alionekana akitiririkwa na machozi huku akijipanuza na kuachia ujumbe wa shukrani kwa Mungu kwa kumpa neema katika maisha licha ya ukakasi mwingi ambao umekuwa ukimzingira tangu Februari akihusishwa na sakata la kifo cha aliyekuwa rafiki yake mbunifu wa mapambo, Jeff Mwathi.

“Ee Baba wa mbinguni, asante Bwana kwa baraka ulizonipa maishani mwangu. Ulinipa zaidi kuliko vile ningeweza kufikiria. Ulinizunguka na watu ambao walinitazama kila wakati. Ulinipa familia na marafiki ambao hunibariki kila siku kwa maneno na vitendo vyema. Waliniinua juu kwa njia ambazo ziliweka macho yangu kwako na kuifanya roho yangu kuongezeka,” Fatxo aliandika.

Wiki mbili zilizopita, Idara ya DCI ambao walikuwa wanachunguza kesi ya mauaji ya Mwathi walitoa taarifa kwamba uchunguzi huo umekamilika na faili imewasilishwa kwa DPP kutathmini kama watuhumiwa watafunguliwa makosa.

Lakini katika taarifa hiyo ambayo iliwashangaza wakenya wengi ambao wamekuwa wakitaka Jeff kupata haki, DCI walionekana kuashiria kwamba huenda Fatxo na wenzake hawakuhusika katika mauaji ya Jeff kama ilivyoripotiwa awali.

Sasa Fatxo anamshukuru Mungu kwa kumlinda katika mzunguko huo wote wa  maneno dhidi yake ambapo amekuwa akionekana mbaya baadhi wakimtaja kama mlawiti.

“Pia asante Bwana kwa kuniweka salama. Ulinilinda na mambo mengi. Ulinisaidia kufanya maamuzi bora na kunipa washauri wa kunisaidia na maamuzi magumu ya maisha. Ulizungumza nami kwa njia nyingi sana hivi kwamba siku zote nilijua kuwa uko pamoja nami. Na Bwana, ninashukuru sana kwa kuwaweka wale walio karibu nami salama na kupendwa. Natumai kuwa utanipa uwezo na akili ya kuwaonyesha kila siku ni muhimu sana. Natumaini kwamba utanipa uwezo wa kuwapa wema sawa na wao wamenipa.”

Kando na shukrani hizo, Fatxo pia alikuwa na ombi kutoka kwa Mungu;

“Bwana, nifundishe kukupa moyo wa shukrani na sifa katika uzoefu wangu wote wa maisha ya kila siku. Nifundishe kuwa na furaha siku zote, kuomba bila kukoma, na kushukuru katika hali zangu zote.”

 

View Comments