In Summary

• Pia alikiri kuwa Wakenya kadhaa bado wamekuwa wakimtumia msaada wa kifedha miezi kadhaa baada ya kuenda viral.

Colonel Mustafa
Image: Screengrab

Baada ya Wakenya kuibua wasiwasi wao kuhusu uwepo wa rapa wa muda mrefu Colonel Mustafa hata baada ya kuchangishwa hela ndefu, msanii huyo sasa ameibuka kuzungumzia kimya chake.

Baadhi ya watu mitandaoni walidai kwamba licha ya msanii huyo kuchangiwa pesa ili kujikwamua kiuchumi na hata kuendeleza biashara ya duka lake la nguo na viatu katika mtaa wa Chokaa, karibu na Kayole, bado duka hilo limesalia mahame.

Kufuatia wasiwasi huo, rapper huyo amejitokeza kueleza hali ilivyo huku akikanusha madai kuwa duka hilo lilikuwa limefungwa kabisa.

“Shop kweli imekuwa ikifungwa lakini si ati tumefunga shop mambo yamekuwa mengi sana. Bado nilikuwa nashughulika na mama tulikuwa tunangoja baada hio radio therapy tufanye pediscan. Hicho ndicho kitu kimekuwa kikinifanya nisipatikane sana kazini pale kwenye duka,” alisema katika mahojiano na chaneli ya Mungai Eve.

“Apart from that mambo ya muziki na pia nimekuwa na shows nyingi nafanya na sijapata mtu mwenye uwezo kumuweka pale mwenye naamini kabisa anaezania kazi mpaka mimi mwenyewe nirudi,” aliongeza.

Pia alikiri kuwa Wakenya kadhaa bado wamekuwa wakimtumia msaada wa kifedha miezi kadhaa baada ya kuenda viral baada ya video yake akifanya kazi ngumu ya mjengo kuenezwa mitandaoni na kuvutia huruma kutoka kwa mashabiki na wahisani wema.

Mustafa alisema kuwa safari ya mama yake kupona saratani inaendelea vizuri na kwa sasa anafanya mazoezi ili kurejesha nguvu zake za kimwili. Akiwa mhudumu, pia amefunzwa jinsi ya kumshughulikia mgonjwa wa saratani.

“Alianza kufanyia mazoezi zumba. Tumefanya radio therapy kama 23 sasa tunafaa kufanya saa hizi ni pediscan ya kuonyesha mwili mzima ile cancer kama ilitoka yote kama ilibaki kidogo,” alifafanua.

Rapa huyo alisambaa mitandaoni mwezi Mei mwaka huu baada ya video yake akifanya kazi ya mjengo kuvuja mtandaoni. Wakati wa mahojiano, alifichua kwamba alijaribu kuweka jambo hilo siri kwa takriban mwaka mmoja.

Wakenya walichanga kwa wingi pesa kwa ajili yake pamoja na wenzake katika tasnia ya muziki.

View Comments