In Summary

• Alikuwa amepinga kukutwa na hatia na kuhukumiwa katika sakata ya Sh313M ya mahindi katika Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Mbunge wa Sirisia John Waluke na mshirika wake Grace Wakhungu
Image: STAR

Mbunge wa Sirisia John Waluke ameachiliwa kwa dhamana ya Shilingi miloni 10 akisubiri kusikizwa kwa rufaa aliyowasilisha.

Alikuwa amepinga kukutwa na hatia na kuhukumiwa katika sakata ya Sh313M ya mahindi katika Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Majaji wa Mahakama ya Rufaa Asike Makhandia, Sankale Ole Kantai na Grace Ngenye walisema mbunge huyo ana njia mbadala ya kulipa bondi ya Shilingi milioni 20 akisubiri kuamuliwa kwa rufaa yake.

Waluke kupitia kwa mawakili wake Otiende Amolo na Elisha Ongoya alikuwa amewaambia majaji wa mahakama ya rufaa kwamba Shilingi milioni 313 zilizounda msingi wa hukumu yake zililipwa kihalali yeye na Wakhungu.

Walisema rufaa yao ina nafasi kubwa ya kufaulu kwani pesa hizo zililipwa kihalali kufuatia tuzo ya usuluhishi ambayo ilithibitishwa na mahakama ya Juu dhidi ya NCPB kwa kukiuka kandarasi.

Maagizo ya msuluhishi hayajawekwa kando lakini NCPB iliwasilisha rufaa ambayo imekuwa ikisubiriwa katika Mahakama ya Rufaa tangu 2012.

Mawakili wa Waluke pia waliteta kuwa mteja wao anadaiwa Sh600M lakini walilipwa nusu tu ya pesa hizo.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma katika nyongeza ameitaka Mahakama ya Rufaa kutompa Waluke dhamana.

DPP kupitia kwa Alexander Muteti aliwaambia Majaji wa mkata rufaa Asike Makhandia, Sankale Ole Kantai na Grace Ngenye kwamba waluke anafaa kusalia gerezani kwani ameshindwa kushawishi mahakama kuhusu ‘hali za kipekee’ zilizopo ambazo mahakama inaweza kuzingatia ili ombi lake la dhamana liruhusiwe.

Aliteta kuwa Waluke alipatikana na hatia ipasavyo na kuhukumiwa na hajathibitisha kwamba rufaa yake pia huenda ikafaulu.

"Rufaa yake haina matumaini. Mahakama haina msingi wa kuvuruga matokeo haya. Kwa kuwa mahakama hii imeundwa ipasavyo, hakuna uwezekano kwamba suala hili litacheleweshwa,” alisema Muteti.

Waluke na mshirika wake wa kibiashara Grace Wakhungu walirudishwa gerezani na mahakama kuu baada ya kuafiki uamuzi wa mahakama ya hakimu mkazi uliowapata wawili hao na hatia ya kujipatia Sh313M kwa njia ya ulaghai kutoka kwa wakala wa serikali.

View Comments