In Summary

•Wazazi wanasema kuwa licha ya kupatwa na kiwewe cha akili baada ya kupoteza watotot wao shule hiyo haijafuatilia kuwafariji wala kuwafidia.

•Wazazi hao wanataka serikali kuwafidia kwa  kuweka watoto wao kwenye mazingira hatari, yenye kasoro na mabaya pale shuleni.

Waziri wa Elimu George Magoha, DP Ruto na gavana Wycliffe Oparanya wakitembelea wanafunzi ambao walinusurika kwenye mkasa wa mkanyangano mwaka jana
Image: DPPS

Wazazi wa wanafunzi 15 walioaga dunia kwenye mkasa wa mkanyangano uliotokea katika shule ya msingi ya Kakamega mwezi Februari mwaka uliopita  wamepeleka kesi mahakamani wakitaka kufidiwa.

Wazazi hao wanataka serikali kuwafidia kwa  kuweka watoto wao kwenye mazingira hatari, yenye kasoro na mabaya pale shuleni.

Kulingana na makaratasi ya kortini, wazazi hao wamedai kuwa watoto wao walikuwa wenye afya na walionyesha dalili za kuwa watu muhimu kwenye jamii ila maisha yao yalikatiwa ghafla kufuatia kutowajibika kwa uongozi wa shule hiyo.

Ambao walitakiwa kujibu mashtaka ni pamoja na mwenyekiti wa bodi ya shule husika, mkuu wa elimu katika kaunti ya Kakamega na mwanasheria mkuu.

Wanafunzi ambao walipoteza maisha yao walikuwa  kutoka darasa la nne na l a tano na walikuwa na umri wa kati ya miaka 9 na 12.

15 hao walikuwa Jane Kiverenge, Bertha Munywele, Salima Olaso, Verm Prince, Samuel Simekha, Fidel Atamba, Catherine Aloo, Joseph Mutsami, Venessa Andeso, Antonatte Khayumbi, Lydia Laventa, Prudence Eliza, Simon Waweru, Nicole Achola na Junne Nakhumicha.

Wazazi wa wanafunzi hao wamedai kuwa mkasa huo ulitokea kwa sababu shule hiyo ilishindwa kulinda wanafunzi wake na kwa hivyo wasimamizi ni wa kulaumiwa.

Walitaja idadi kubwa ya wanafunzi, ngazi nyembamba na zenye giza pale shuleni kutokuwa na uwezo wa kudhibiti wanafunzi wale.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Novemba 29 mwakani.

Wazazi wanasema kuwa licha ya kupatwa na kiwewe cha akili baada ya kupoteza watoto wao shule hiyo haijafuatilia kuwafariji wala kuwafidia.

Wamesema hawana budi ila kuchukua mkondo wa kisheria.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments