In Summary

• Manchester United na Chelsea zimetajwa kuwa mstari wa mbele kuwinda saini ya Messi ambaye anatarajiwa kuondoka PSG mwishoni mwa msimu.

Mchezaji wa kimataifa wa Argentina Lionel Messi akisherehekea bao
Image: Instagram

Taarifa za kushtusha sasa zimefichua kuwa Lionel Messi ameibuka kwenye darubini za vilabu viwili vya Ligi Kuu ya Uingereza vinavyozitaka huduma zake pindi atakapoondoka PSG.

Mshambulizi huyo wa Paris Saint-Germain atakuwa mchezaji huru mwishoni mwa msimu huu. Alisaini mkataba wa miaka miwili alipojiunga na wababe hao wa Ufaransa akitokea Barcelona mwaka jana.

Kulingana na taarifa kutoka kwa jarida la El Nacional ambazo zimesambazwa pakubwa mitandoni, Manchester United na Chelsea wana nia ya kupata huduma ya nyota huyo msimu ujao.

Kutokana na kanuni za mishahara ya La Liga, Messi alijiunga na PSG msimu uliopita baada ya Barcelona kushindwa kumuongezea mkataba mchezaji huyo. Alivumilia msimu mgumu wa kwanza nchini Ufaransa, akifunga mabao 11 na kutoa asisti 15 katika mechi 34.

Hata hivyo, Messi amerejea katika kiwango chake msimu huu na amefanikiwa kufunga mabao tisa na kutoa pasi za mabao kumi katika michezo 15 hadi sasa katika kampeni zinazohusisha timu ya PSG.

United wana nia ya kuongeza washambuliaji upande wao. Cristiano Ronaldo yuko katika hali tata na klabu hiyo na huenda yuko njiani kuondoka. Alifungiwa nje ya mechi ya hivi punde zaidi ya Mashetani Wekundu dhidi ya Chelsea mnamo Oktoba 22.

Kujiunga na Ligi Kuu ya Premia pia kutampa Lionel Messi nafasi ya kujibu mashaka ya muda mrefu kuhusu jinsi atakavyofanya katika ligi hiyo yenye ushindani zaidi duniani.

View Comments