In Summary

• Baadhi ya wachanganuzi wa soka walihisi kwamba UEFA ilikuwa inajaribu kumpaisha sana licha ya kutokuwa na msimu wa kufana akiwa PSG.

Image: INSTAGRAM// LIONEL MESSI

Nahodha wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi amefunguka baada ya kuteuliwa katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora Uropa.

Messi alisema kwamba kwa sasa hazingatii sana kushinda taji lolote la kibinafsi kwani yeye ndoto yake ni kama ilikamilika aliposhinda kombe la dunia mwaka 2022 nchini Qatar – kombe ambalo alisema alikuwa analifukuzia kwa muda mrefu na ndilo pekee lililokuwa limekosekana kwenye rafu yake ya mataji.

Mchezaji huyo alipoulizwa kuhusu uwezekano wake wa kuweka rekodi kwa kushinda taji la Ballon d’Or kwa mara ya nane, alisema kwamba wala hatilii maanani sana kwani tayari ameshashinda mara 7 na ikitokea ameshinda ni sawa na asiposhinda bado hatohisi chochote.

”Unaweza kufikiria kwamba baada ya kushinda Kombe la Dunia, ambalo ndilo jambo pekee nililokuwa nikikosa, sifikirii zaidi kuhusu Ballon d’Or. Kombe la Dunia lilikuwa tuzo yangu kubwa zaidi, sasa ninafurahia wakati huu na kwa uaminifu sifikirii juu yake. Nikishinda, vizuri, na nisiposhinda basi hakuna kitakachotokea,” Messi alisema.

Licha ya kuondoka katika soka la Ulaya kwa mara ya kwanza katika takribani miaka 20 iliyopita, mchezaji huyo bado aliteuliwa miongoni mwa wengine kuwania tuzo ya mchezaji bora barani Ulaya.

Baadhi ya wachanganuzi wa soka walihisi kwamba UEFA ilikuwa inajaribu kumpaisha sana licha ya kutokuwa na msimu wa kufana akiwa PSG.

Kwa mujibu wa UEFA, Orodha fupi ya awali ya wachezaji ilichaguliwa na kikundi cha utafiti wa kiufundi cha UEFA kulingana na uchezaji wao katika msimu wa 2022/23 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Wagombea watatu bora kisha walipigiwa kura na baraza la majaji lililoundwa na makocha wa vilabu vilivyocheza hatua ya makundi ya UEFA Champions League 2022/23, UEFA Europa League na UEFA Europa Conference League, pamoja na makocha wa timu za taifa za wanaume, timu za vyama vya wanachama wa UEFA.

Kundi la waandishi wa habari waliochaguliwa na Vyombo vya Habari vya Michezo vya Ulaya (ESM) pia walikuwa sehemu ya majaji.

Makocha na waandishi wa habari walitakiwa kuchagua wachezaji wao watatu bora kutoka kwenye orodha hiyo kwa kuwagawia pointi tano, pointi tatu na pointi moja mtawalia.

Matokeo ya mwisho yalitokana na jumla ya kura zilizopigwa na makocha na waandishi wa habari. Makocha hao hawakuruhusiwa kuwapigia kura wachezaji wa timu yao wenyewe.

 

View Comments