
Kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) Rigathi Gachagua amemtuhumu Naibu Rais Kithure Kindiki kuwa ndiye aliyehusika na ghasia zilizoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga serikali mwezi uliopita.
Akizungumza mjini Boston, Marekani, Gachagua alidai kuwa Kindiki alipokea Shilingi milioni 60 kutoka kwa Rais William Ruto ili kufadhili kampeni ya siri inayolenga kumharibia sifa pamoja na washirika wake katika eneo la Mlima Kenya.
"Waliwalipa wahuni kusababisha vurugu na kutuharibia jina ili Wakenya watugeukie. Lakini Wakenya si vipofu; wanaona udanganyifu huu," Gachagua alidai.
Aidha, alimlaumu Kindiki kwa kutumia fedha za umma chini ya mwamvuli wa uwezeshaji kuanzisha kampeni za mapema kuelekea uchaguzi wa 2027.
"Fedha anazozurura nazo kwa helikopta zingeweza kurekebisha hospitali na shule. Badala yake, zinatupwa hovyo kwa jina la uwezeshaji. Lakini vijana wanaangalia kwa makini," alisema.
Gachagua aliwasilisha maono yake ya siku 100 za kwanza iwapo atachaguliwa kuwa rais, akiahidi kukomesha mauaji ya kiholela, kurejesha uhuru wa taasisi na kufufua huduma muhimu za umma.
"Kipaumbele changu cha kwanza kitakuwa kukomesha utekaji na mauaji ya kiholela na kurejesha utawala wa sheria. La pili litakuwa kuruhusu taasisi kama Bunge kuwa na uhuru ili kufanya maamuzi yenye ufanisi," alisema.
Gachagua pia alimshambulia Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang'ula, akimtuhumu kwa kukosa kuwa na msimamo wa kati katika ofisi yake kwa kuendesha kampeni waziwazi za kumpigia debe Rais Ruto.
"Spika anapaswa kuwa mtu wa kati, lakini tulicho nacho sasa ni mtu anayempigia debe rais, kuhudhuria harambee na kutoa vitisho vya kisiasa. Hiyo si nafasi ya kiongozi wa Bunge mwenye msimamo wa kati," alisema.
Wakati huo huo, Mbunge wa Naivasha Jayne Kihara ametakiwa kufika mbele ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhojiwa kuhusiana na madai ya uchochezi.