
Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alifanya mazungumzo ya wazi na wanajumuiya wa Abagusii jijini Seattle, Washington, Marekani, mnamo Julai 15, 2025.
Gachagua alisema alifurahishwa kukutana na "binamu zake" walioko Marekani.
“Jioni ya leo, nimefurahia kukutana na kufanya mazungumzo ya dhati na binamu zangu kutoka jamii ya Abagusii hapa Seattle, Washington,” alisema Gachagua.
“Nina furaha kuwa wanatambua changamoto ambazo nchi yetu inapitia na pia kujitolea kwao kusaidia mageuzi chanya,” aliongeza.
“Ni jambo la kutia moyo kuona wanajamii wetu wakikusanyika kwa nia njema, matumaini, na tamaa ya pamoja ya kuchangia katika siku bora za baadaye.”
Gachagua alianza ziara yake ya Marekani mnamo Julai 9.
Hii ni safari yake ya kwanza nje ya nchi tangu aondolewe madarakani.
Gachagua alipanga kutembelea miji kadhaa katika ziara hiyo ya miezi miwili, ikiwemo Dallas, California, Seattle, Boston na Baltimore.
Katika ziara hiyo, Gachagua atafanya mikutano mbalimbali ya hadhara na kushiriki mikusanyiko ya kijamii ili kuendeleza ajenda yake kwa jumuiya ya wakenya waishio ughaibuni.
Pia anatarajiwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji wa Marekani kama sehemu ya kampeni pana ya kuonesha upinzani kama mbadala wa kuaminika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Vyanzo vya karibu vimeeleza kuwa Gachagua anatarajiwa kufanya mikutano na wawekezaji wanaoripotiwa kuwa na nia ya kushirikiana na upinzani kabla ya uchaguzi.
Hata hivyo, alielezea wasiwasi wake kuhusu kile alichokitaja kama njama za serikali za kuzuia safari zake nje ya nchi.
Gachagua ni mshirika muhimu katika muungano wa upinzani unaojumuisha kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa People’s Liberation Party Martha Karua, kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, na aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i.
Ziara yake inafanyika siku chache tu baada ya Matiang’i kuanza kampeni yake ya urais ya 2027 katika uwanja wa kimataifa kwa kufanya mkutano wa hadhara na wakenya waishio ughaibuni huko Texas, Marekani.