Mchekeshaji wa Kenya mwenye makazi yake Marekani, Elsa Majimbo amefichua kwamba kuna baadhi ya watu wanaojaribu kumtumia pesa kupitia mtandao wa Instagram.
Majimbo aliweka video kwenye instastory yake akisema kwamba amepokea ujumbe kutoka kwa Instagram kuhusu baadhi ya watu wanaojaribu kumtumia pesa, na kusema kwamba haliafiki jambo hilo.
Kutokana na hilo, Majimbo aliwaonya vikali watu na mashabiki wake ambao wanajaribu kumtumia pesa kama zawadi akisema kwamba hahitaji pesa zao.
“Instagram imeniarifu kwamba kuna watu wanajaribu kunitumia pesa. Baadhi yenu mnataka kunipa pesa kama zawadi. Yaani mnajaribu kuhakikisha kwamba ninakubali ombi la kupokea pesa kutoka kwenu? Hapana, tusifanye hivyo ndugu zangu,” Majimbo alisema.
“Isiwe kwamba mnajaribu kunilipa haswa inapokuja katika maudhui yangu ambayo ninachagua kuwafanyia na nyinyi mnachagua kuyakubali. Kitu msichokujua haswa katika ukurasa wangu ni kwamba sisi wote tunachagua kuwa hapa na hivyo nisingependa hilo kugeuka kuwa ni niia ya kunilipa, hapana. Nawapenda sana lakini wekeni pesa zenu kwenye mifuko yenu,” aliongeza.
Wiki chache zilizopita, mrembo huyo alithibitisha kuachana na aliyekuwa mpenzi wake DJ Hkeem.
Mtayarishaji wa maudhui huyo alitaja kutomwamini mpenzi wake baada ya kisa kilichotokea alipokuwa ameenda kwa mahojiano.
Alisimulia mlolongo wa matukio ambayo yalisababisha kutengana katika video iliyotumwa kwenye kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii.