Mkurugenzi Mtendaji wa halimashauri ya mirabaha na hakimiliki kwa kazi za kisanaa nchini, MCSK Ezekiel Mutua ametofautiana vikali na pendekezo la Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria la kutaka malipo ya mirabaha yalipwe kupitia e-Citizen.
Mutua alisema kazi ya serikali inapaswa kuwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanamuziki kuimarika na kisha kukusanya ushuru unaotokana na malipo ya mirabaha.
“Waziri anaposema kuwa Serikali itakusanya mirabaha ya wasanii kupitia e-Citizen, huo ni ujinga wa hali ya juu. Muziki ni talanta kama mpira wa miguu au riadha. Je, Serikali inakusanya malipo ya wanasoka au wanamichezo kupitia e-Citizen?” Mutua aliuliza.
"Muziki ni haki ya kibinafsi na Serikali inaweza tu kupata ushuru unaotokana na malipo ya mirahaba, lakini haiwezi kudaiwa kusimamia hakimiliki kwa niaba ya wanamuziki," Mutua aliongeza.
Haya yanajiri baada ya Kuria kusema kuwa serikali inanuia kurekebisha Sheria ya Hakimiliki ili kuunda Shirika la Usimamizi wa Pamoja (CMO).
Waziri huyo alisema wanamuziki watasajiliwa na serikali na wataangalia jinsi pesa zinavyokusanywa kupitia e-Citizen.
Hii ni baada ya serikali ya Ruto kuanzisha nambari moja ya malipo ya paybill kwa huduma zote za serikali.
Siku chache zilizopita, serikali kupitia kwa katibu katika wizara ya elimu, Bellio Kipsang, ilitoa notisi kwa shule zote za kitaifa kutuma maelezo yao ili kuhakikisha kwamba karo zote zinalipwa kupitia eCitizen kupitia kwa nambari hiyo moja.
Hata hivyo, baadhi ya washikadau katika sekta ya elimu walielekea mahakamani na kupinga agizo hilo ambalo mahakama ililisimamisha kwa muda.