Mashabiki wa Nicki Minaj wamepatwa na hasira baada ya tamasha la rapper huyo wa Marekani kwenye uwanja wa Co-op Live wa Manchester kusitishwa dakika za mwisho, kufuatia kukamatwa kwake kwenye Uwanja wa Ndege wa Amsterdam wa Schiphol.
Minaj alikamatwa kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya kabla ya kutozwa faini na kuruhusiwa kuendelea na safari yake, polisi wa Uholanzi walisema.
Hata hivyo, hakufika Manchester kwa wakati kwa ajili ya tamasha lake Jumamosi, ambalo liliahirishwa kwani takriban mashabiki 20,000 walikuwa uwanjani wakimsubiri kupanda jukwaani.
Walijumuisha Imogen Papa, 18, kutoka Newton-le-Wilows huko Merseyside, ambaye alisema "alikuwa amekasirika sana".
"Nilitumia Pauni 150 kwa tikiti yangu na nikaweka siku ya kupumzika kwa ajili yake, na tulikaa hapo kwa takriban saa tatu tukingoja na tukaambiwa halitafanyika," alisema. "Nimekatishwa tamaa."
Ellis Day, 17, kutoka Cheshire, alisema "amehuzunika kweli".
"Tumekuja hapa, tulitumia siku nzima kujiandaa, kuona hii ikitokea.
"Inasikitisha sana tunapoweka matumaini yetu na kutumia pesa, na tunaambiwa dakika za mwisho kabisa kwamba hatajitokeza."