Mchekeshaji Mulamwah ni mwathirika mwengine katika msururu wa watu wengi ambao wamekuwa wakipoteza akaunti zao za TikTok katika mazingira yasiyojulikana.
Mulamwah alichapisha ujumbe akithibitisha kupotea kwa akaunti yake kwenye mtandao huo wa video fupi, katika kile kilichoonekana kama ni kufungiwa.
Mpaka wakati inatoweka, akaunti ya Mulamwah ilikuwa imejikusanyia jumla ya wafuasi milioni 1.1 na hilo lilionekana kuwa pigo kuu kwa mchekeshaji huyo.
Hata hivyo, Mulamwah alijitia hamnazo akisema kwamba kwa sasa hana akaunti katika mtandao huo ila anashukuru Mungu akaunti yake ya benki haijaathirika kwa njia yoyote ile.
“Bora akaunti yangu ya benki ya Equity iko sawa, tunasonga mbele,” Mulamwah alisema.
Pia alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha mashabiki wake kwamba kwa sasa hayuko tena kwenye TikTok na wakuwe macho wasije wakahadaiwa kwani kuna walaghai wengi wameshaanza kufungua akaunti kwa jina lake wakijifanya kuwa yeye.
“Kwa sasa sina akaunti kwenye TikTok, msitapeliwe huko,” aliongeza.
Katika miezi ya hivi karibuni, watu wengi wamekuwa wakilia katika mitandao ya kijamii baada ya kufungwa kwa ghafla kwa akaunti zao za TikTok bila kupatiwa sababu.
Baadhi ya walioonesha kufadhaika kwao baada ya akaunti zao kufungwa ni pamoja na Faustine Baba Talisha ambaye yake ilifungwa saa chache baada ya kufikisha wafuasi milioni moja, Njoki Murira na wengine.