Mwimbaji mkongwe wa Jamaica Sean Paul Ryan Francis Henriques OD almaarufu Sean Paul atafanya ziara ya Kenya mwishoni mwa mwaka huu wa 2024.
Mnamo siku ya Jumatatu, Oktoba 28, msanii huyo wa dancehall mwenye umri wa miaka 51 alithibitisha kwamba atatumbuiza katika jiji la Nairobi mnamo mwezi Desemba.
Sean Paul aliwataka mashabiki wake kuandaa tiketi zao huku wakisubiri kumtazama akitumbuiza moja kwa moja jukwaani.
“Nani kasema siji jijini Nairobi? Pata tiketi yako sasa!” Sean Paul alisema Jumatatu jioni kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Mwimbaji huyo aliambatanisha chapisho lake na kiungo ambapo mashabiki wanaweza kupakua tikiti zao kutoka.
Kulingana na bango la shoo hiyo lililosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, staa huyo wa dancehall atatumbuiza katika jiji kuu la Kenya mnamo Desemba 1, 2024.
Sean Paul atatumbuiza pamoja na baadhi ya wasanii wa Kenya wakiwemo Redsan, G-Money, CNG, Dream, Sir Effexy, Mish, ZJ Heno, Motif Di Don na kundi la wasanii wa arbantone.
Tikiti za tamasha hilo zinauzwa kuanzia Sh3000 kwa shabiki wa mapema hadi 120,000 kwa kundi la kitengo cha dhahabu la watu 6.