MSANII na mjasiriamali Esther Akoth Kokeyo, maarufu
kama Akothee amedokeza kwamba bado hajafa moyo katika kusimika penzi lake
kwenye ndoa ya harusi.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Akothee alichapisha
picha zake za zamani na kuweka wazi kwamba kama kuna jambo hawezi kuchoka
kulifanya, basi ni kufunga harusi.
Alisema kwamba hivi karibuni, atafunga harusi
nyingine ya 3 ambayo aliitaja kuwa itakuwa ya mwisho kabisa katika maisha yake
ya kusaka mapenzi.
Mama huyo wa watoto 5 alidokeza kuwa ndoa hiyo ya
tatu itakuwa baina yake na mpenzi wake wa muda mrefu, Nelly Oaks ambaye
alimtaja kama ‘partner in crime’.
“KUOLEWA
KWA AKOTHEE NI CONSTANT. Harusi yangu ijayo ya 3 na pengine ya mwisho itakuwa
nzuri zaidi kwa sababu nitakuwa nikioana na mpenzi wangu katika uhalifu,”
Akothee alisema.
Akionekana kutupa dongo kwa penzi lililosambaratika
na wapenzi wa awali, alisema kuwa wapenzi wake – akiwemo Denis Schweizer
maarufu kama Mr Omosh, walikuwa ni walanguzi wa mapenzi tu.
Hata hivyo, alionesha Imani ya ndoa yake ya mwisho na
Nelly Oaks kuwa na mafanikio akisema kuwa isipofanya kazi bado atarudi sokoni
kujaribu harusi kwa mara ya 4.
Aliwataka mashabiki wake kutolalamika kuhusu idadi ya
harusi atakazofanya, akiwaambia kwamba lao litakuwa tu kununua vitenge na kwa
wale watakaokuwa mbali yao itakuwa kununua bundles ili kufuatilia mtandaoni.
“Hawa
wengine walikuwa Criminal wa mapenzi. Sasa hii ni kweli halisi. Na hii ya tatu
isopofanya vizuri, Tutakuwa na another last one wewe kazi yako iwe ni kushona
kitenge na bundles,” Akothee alisema.
Itakumbukwa mwaka jana, Akothee alisimamisha jiji la
Nairobi na mitandao ya kijamii mnamo Aprili alipoamua kufunga harusi ya
kifahari.
Harusi hiyo iliandaliwa kwa mtindo wa kifahari ambapo
alisema ‘NDIO’ kwa mpenzi wake wakati huo, raia kutoka Uswizi, Denis Schweizer
aliyekuwa amempa jina Mr Omosh na hata kumfungulia akaunti za mitandao ya
kijamii kwa jina hilo.
Hata hivyo, miezi 5 baadae, ndoa hiyo ilisambaratika
na ilimchukua Akothee muda mrefu kukubali ukweli huo na hata kuusema wazi kwa
mashabiki wake mtandaoni.