MSANII na mjasiriamali Esther Akoth maarufu kama
Akothee amechagua kumsherehekea tiktoker Rachael Otuoma kwa upendo wa kipekee
aliomuonyesha marehemu mumewe Ezekiel Otuoma hadi kifo chake.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Akothee aliwakosoa
baadhi ya watu ambao walianza kuandika jumbe za kuhoji jinsi Otuoma alipata
kifo chake wakati mkewe akiwa kwenye tafrija ya kusherehekea siku yake ya
kuzaliwa.
Akothee alihisi hoja kama hizo ni za kumkosea heshima
Rachael, haswa kipindi hiki aqnapoomboleza, akiwataka watuy kuangalia zaidi kwa
yale mazuri ambayo amemfanyia mumewe kwa miaka 4 aliyougua.
“Mitandao
ya kijamii imeunda jukwaa ambapo mtu yeyote anaweza kuchapisha chochote, mara
nyingi bila huruma au akili ya kihisia. Uzembe na kutojali unaoonyeshwa na
baadhi ya watu, hata wakati wa huzuni, unaweza kuwa mwingi. Watu wanaonekana
kushindana juu ya kila kitu, hata katika kifo, na kusahau ubinadamu unaotufunga
sisi sote,” Akothee alifoka.
Alisema yeye ameamua kumpa maua mrembo Rachael kwa
kudhihirisha bayana kwamba kauli ya “katika ugonjwa na katika afya hadi kifo
kitutenganishe” inawezekana.
“Katikati
ya machafuko haya, ninataka kutambua na kuheshimu nguvu na uthabiti wa Rachel
Otuoma. Mwanamke huyu wa ajabu anatoa mfano wa maana halisi ya "katika
ugonjwa na afya, mpaka kifo kitakapotutenganisha." Kusimama kando ya mume
wake katika nyakati za hatari zaidi kulihitaji nguvu nyingi za kihisia,
kisaikolojia na kiakili. Wachache wangekuwa na ujasiri wa kufanya kile
alichofanya, kujali bila ubinafsi na kwa upendo,”
Akothee alimsifia Rachael.
Alisema kwamba mambo ambayo Rachael alikuwa
akimfanyia Otuoma, japo madogo na ya kawaida yalikuwa ndio furaha na faraja
kubwa kwa marehemu.
“Raheli,
kujitolea kwako bila kuyumba ni ushuhuda wa nguvu ya upendo. Kila nilipokuona
unamchezea mumeo, niliona furaha na faraja iliyomletea, unaweza usijue lakini
unaongeza pumzi yake kwa tabasamu hilo,” alisema.
“Kwa
wale wanaokosoa na kuhukumu, kumbuka kuwa huzuni ni ya mtu binafsi, na heshima
ni sifa ambayo sisi sote tunapaswa kuidumisha. Raheli, jifariji kwa kujua
kwamba ulitoa bora yako na kuheshimu nadhiri zako kwa ukamilifu,”
Akothee aliongeza.