MTANGAZAJI nguli katika kuongoza vipindi vya miziki ya Reggae, Tallia Oyando maarufu kama Night Nurse ametangaza kufunga ukurasa wa safari yake ya utangazaji na runinga ya Citizen.
Kupitia chapisho la kipekee kwenye ukurasa wake wa Facebook
alasiri ya Jumatatu, Oyando alisema kwamba miaka 8 katika kituo hicho cha
runinga chini mwavuli wa Royal Media imemtosha na sasa ni muda wa kufungua
ukurasa mwingine.
Aliwashukuru mashabiki wake wa kipindi cha Reggae, ‘One
Love’ na kusema kwamba kuondoka kwake si kwaheri bali ni mapumziko ya muda
kabla ya kuibuka tena.
“Baada
ya miaka 8 maridadi ya mapenzi, muziki, na familia kwenye One Love katika
Citizen TV, ni wakati wa sura mpya. Asante kwa kila mmoja wenu ambaye alifanya
safari hii isiyosahaulika. Kama Joseph Hill alivyosema, 'Upendo hung'aa zaidi
kuliko jua la asubuhi.' Hii sio kwaheri, mambo makubwa yanakuja. Tukutane kwa
kipindi cha mwisho cha @onelovectv kwenye @citizentvkenya Jumamosi hii One
Love, daima na milele,” Oyando alisema.
Mrembo huyo aliwaacha mashabiki wake na ujumbe kutoka
kwa wimbo maarufu wa Redemption Song kutoka kwa gwiji wa utunzi wa miziki ya
Reggae aliyewahi kuishi, Bob Marley.
“Ninapowaaga,
ninawaacha na huu ujumbe wa kujikomboa kutoka kwa umaskini wa kifikira, hakuna
mwingine bali ni sisi tunaoweza kujikomboa. Acha muziki uendelee kuzikomboa
roho zenu, kuinua mioyo yenu na kutuunganisha sisi sote. Hii si kwaheri, ni
kusherehekea muziki, kumbukumbu na ufamilia tuliounda pamoja. Kama nyimbo
ambazo tulizienzi pamoja, upendo wangu kwenu hautayeyuka,”
Oyando aliongeza.
Oyando alianza kuongoza kipindi hicho cha kila usiku
wa Jumamosi kwenye runinga ya Citizen mnamo Oktoba 22, 2016 ambapo alikuwa
akishirikiana na Coco Soboo Moto.