
MCHUNGAJI wa kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a ameendeleza mashambulizi yake dhidi ya baadhi ya Wakenya ambao wamekuwa wakimshambulia mitandaoni.
Ng’ang’a amekuwa akishambuliwa mitandaoni kwa takribani wiki
3 sasa baada ya video kuibuka mitandaoni ikimuonyesha jinsi alimfukuza kwa
dharau mwanamke mmoja kutoka kanisa lake.
Katika video hiyo, mwanamke huyo kwa jina Milka Moraa Tegisi
alikuwa ameenda kutafuta msaada wa kodi ya nyumba yake ambayo ilikuwa
imefungwa.
Ng’ang’a alimlipua kwa ukali akimwambia kwamba hapo si pa
kutafuta msaada ya hata kumuelekeza kuenda kutafuta msaada kwa nyumba za bei
nafuu zinazojengwa na serikali kupitia mpango wa Boma Yangu.
Baada ya video hiyo kuibua huruma mitandaoni, afisa mmoja wa
polisi – Sammy Ondimu Ngare, alijitoa kimasomaso kuwaongoza Wahisani wema
kumchangia Moraa hela kwa ajili ya kutatua matatizo yake ya kodi ya nyumba.
Kando na kuongoza michango, Ondimu alimsaidia Milka kupata
kazi katika mgahawa mmoja lakini pia kumkutanisha na waziri wa ardhi Alice
Wahome aliyeahidi kumkabidhi mama huyo nyumba yake kupitia Boma Yangu katika
kipindi cha wiki 2.
Hata hivyo, harakati za afisa huyo wa polisi kumsaidia Milka
zilionekana kumkera mchungaji Ng’ang’a ambaye katika mahubiri yake wikendi
iliyopita, aligeuza mtutu wake wa mashambulizi kwa polisi huyo.
Katika klipu ambayo afisa huyo wa polisi alichapisha kwenye
ukurasa wake wa Facebook, Pasta Ng’ang’a anaonekana akimfokea vikali akimwambia
kwamba yeye hana hata pikipiki wakati yeye [Ng’ang’a] anateleza kwa gari la
kifahari aina ya Lexus.
“Kama ni mtu mwingine
mimi huwa siongei, lakini afisa wa polisi…sasa Ondimu hata ukatokezea hapa,
hata ndevu huna. Hata huna pikipiki wewe, mimi niko na Lexus 600.”
“Tafuta rika lako mcheze
nao, wale wahubiri ambao mmetahiri nao,” Ng’ang’a alihubiri huku
akitoa onyo kali kwa polisi huyo dhidi ya kutojaribu tena wakati mwingine.
Awali, Ng’ang’a alikashifu vikali baadhi ya watu waliokuwa
wakimtupia cheche kwa kitendo alichomfanyia Milka kumfukuza kanisani.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo, alihoji mbona watu
hawazungumzii idadi kubwa ya watu ambao amesaidia katika kanisa lake lakini
hiki kisa kimoja tu ndicho kila mmoja anamhukumu nacho.