
FAITH Kathambi, mwanamke aliyegonga vichwa vya habari takribani mwezi mmoja uliopita katika kaunti ya Kisii akichapwa kwa kushukiwa kuiba unga amepata fursa nyingine ya kuishi maisha mazuri, shukrani kwa Eric Omondi.
Kathambi alikabidhiwa nyumba yake ya kifahari na
mwanaharakati Eric Omondi ambaye amefanya jitihada kumjengea kupitia kwa wakfu
wake wa SisiKwaSisi.
Akitoa taarifa kuhusu ujenzi huo, Eric Omondi aliwashukuru
Watu wote waliochangia katika michango ya kufanikisha ujenzi wa jumba hilo
ambalo alilionyesha kwenye video.
“MUNGU ANASHINDA. TEAM
SISI KWA SISI Tunaweka Historia Polepole lakini Hakika. Kubadilisha maisha na
Kuathiri Jumuiya. Mungu awabariki sana wanaotoa. SHUKRANI KUBWA SANA KWA
@kpfcbuildershardware kwa kutoa Vifaa vyote vya kumalizia nyumba, Mungu ibariki
@kpfcbuildershardware FAITH sio mmiliki wa Ardhi tu bali pia mwenye nyumba.
MUNGU AWABARIKI,” Eric Omondi alisema.
Awali, Omondi aliwataarifu wafuasi wake kwenye Instagram
kwamba Kathambi alikuwa pia amekabidhiwa shamba atakaloliita la kwake.
“Mabibi na Mabwana FAITH
KATHAMBI rasmi ni Mmiliki wa Ardhi kwa Hisani ya SISI KWA SISI… MWENYEZI MUNGU
AWABARIKI KILA ANAYECHANGIA,” Eric alisema.
Taarifa ya Kathambi kunyanyaswa na majirani kwa kudaiwa kuiba
mfuko wa kilo mbili wa unga katika kijiji kimoja kaunti ya Kisii iliangaziwa na
runinga ya Citizen na kuuza huzuni mwingi.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, mama huyo mwenye mtoto mmoja
aliyeonekana akichapwa na mwanamume mmoja kwa madai ya kuiba unga kutoka kwa
mama mkwe alikuwa na tatizo la ulemavu pia.